Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewaagiza Wakuu wa Wilaya wa mkoa huo kufanya kazi kwa kushirikiana kulingana na uwezo wao, huku wakifanya maamuzi sahihi yatakayochochea ukuaji wa maendeleo katika wilaya zao.
Pia ameagiza kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujenga mahusiano mema na chama hicho.
Maelekezo hayo yalitolewa Septemba 5, 2024, wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Mkuu mpya wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, aliyechaguliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo.
Kunenge amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa uadilifu, akieleza kuwa ni muhimu kuondoa urasimu unaoweza kukwamisha juhudi za serikali katika kufanya mapinduzi ya viwanda katika mkoa huo.
” Wakuu wa Wilaya wanatakiwa kusimamia ulinzi na usalama katika maeneo yao,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, ameahidi kufanya kazi kwa mujibu wa kiapo chake, ili kuhakikisha maono ya Rais Samia Suluhu Hassan yanafikiwa.
Mkoa wa Pwani una jumla ya wilaya saba, ambapo katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ,Wilaya za Bagamoyo na Rufiji ndizo zilizopata Wakuu wapya Shaibu Ndemanga amehamishiwa Wilaya ya Bagamoyo, huku Luteni Kanali Fredrick Komba akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji.