Home AFYA NIC YAIGUSA IDARA YA WATOTO MUHIMBILI KWA MSAADA WA MILIONI 20.

NIC YAIGUSA IDARA YA WATOTO MUHIMBILI KWA MSAADA WA MILIONI 20.

Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vifaa tiba, fenicha pamoja na ukarabati wa kliniki ya watoto wenye thamani ya shilingi milioni 20 kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa lengo la kuboresha huduma kwa watoto wanaohudumiwa hospitalini hapo.

Akizungumza leo Septemba, 5 2024 wakati wa kupokea msaada huo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji MNH Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dk. John Rwegasha amesema msaada huo utaimarisha utoaji wa huduma kwa watoto wanaopata changamoto za afya kwani kwa sasa mtoto anayepata dharura akiwa kliniki atapata huduma katika chumba maalum na kurudi nyumbani badala ya kulazwa wodini kama ilivyo kuwa awali.

“Tunawashukuru NIC kwa kuguswa na kuleta msaada huu katika wodi hii ya watoto kwani vifaa hivi vitaleta mabadiliko katika kuwahudumia watoto wanaofika Muhimbili kupata huduma za afya,” amefafanua Dk. Rwegasha

“Malengo ya hospitali ni kuendelea kuifanya Muhimbili kuwa hospitali bora zaidi kwa matibabu ya watoto nchini”, amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano kutoka NIC, Kareem Meshack amesema Muhimbili ni wadau wa karibu hivyo msaada huo umelenga kuimarisha huduma za afya kwa mtoto kwani wao ndio msingi wa maendeleo na uchumi wa taifa la kesho.

“Hii ni moja ya sera yetu ya kurudisha kwa jamii pia tunaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kwamba afya ya mtoto inaimarika na huduma za afya zinapatikana katika mazingira bora na salama,”amesema Kareem.

Naye Mkuu wa Idara ya Watoto MNH Dk. Monica Appolo amesema idara hiyo inahudumia watoto takribani 200 kwa siku hivyo amewaomba wadau, mashirika na watu binafsi kujitokeza kutoa msaada kwa watoto kwani uhitaji ni mkubwa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here