Saidina Msangi, WF, Pwani.
MKUU wa wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti amewaasa watoa huduma za fedha wilayani humo kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kwa kufuata sheria za Serikali ili waweze kutoa huduma za fedha wilayani humo.
Magoti ametoa rai hiyo Septemba, 3 2024 alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha waliofika wilayani hapo kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni awamu ya mwisho ya mfululizo wa programu ya elimu ya fedha kwa umma inayotekelezwa na Wizara ya Fedha.
Amesisitiza kuwa endapo kuna watoa huduma za fedha ambao wanaendesha shughuli zao wilayani humo na hawana leseni wakibainika kutoa mikopo bila kusajiliwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
‘‘Kila mtu afanye kazi kwa kufuata utaratibu hakuna mtu anaweza kupata pesa nje ya utaratibu hivyo taasisi za fedha zinazofanya kazi wilaya ya Kisarawe zihakikishe zimesajiliwa kisheria,’’amesisitiza Magoti.
Pia meipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kwani itawasaidia kuepukana na mikopo umiza pamoja na kutambua umuhimu wa kuweka akiba.
Aidha, Magoti ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanatumia watoa huduma za fedha waliosajiliwa ili kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa.
Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi wa wilaya hiyo Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Stanley Kibakaya amesema kuwa Serikali inatekeleza programu hiyo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya fedha kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha.
‘‘Ni lazima kuwa makini sana katika kupanga matumizi ya fedha, hakikisha mapato na matumizi, matumizi yasizidi, kila fedha unayopata tunza asilimia kumi tuwe na utaratibu wa kuweka akiba katika sehemu rasmi kwani akiba haiozi na kuhakikisha kuwa unapochukua mikopo taasisi hiyo imesajiliwa na ina leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania,’’ amesisitiza Kibakaya.
Amewasisitiza kuwa wasitumie taasisi ambazo hazijasajiliwa na Serikali ili inapotokea changamoto waweze kupata suluhisho kwani kutumia taasisi ambazo hazitambuliki mwananchi atapoteza haki ya msingi ikiwemo kupewa mkopo bila kufuata kanuni za mikopo ikiwemo riba kubwa.