Home KITAIFA KADI JANJA ZA MWENDOKASI ZAZINDULIWA RASMI.

KADI JANJA ZA MWENDOKASI ZAZINDULIWA RASMI.

Dar es salaam

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amezindua Mageti janja na Kadi janja kwenye mwendokasi huku amewataka Watendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha wanafanya mchakato wa haraka kupunguza changamoto ya usafiri inayosababishwa na uhaba wa mabasi hayo .

Agizo hilo amelitoa Septemba 2, 2024 Jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa mfumo wa matumizi ya kadi janja na geti janja ambapo amesema licha ya kuwa na mfumo huo ambao unakwenda kuondoa matumizi ya karatasi lakini ni budi Dart kushirikiana hata na kampuni binafsi za usafiri ili kuleta suluhisho la changamoto ya abiria kukaa zaidi ya masaa kusubiria usafiria huo .

Amesema uzinduzi huo wa kutumia kadi janja ni mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji baada ya kutumia karatasi kwa muda mrefu na utasaidia kupata taarifa za mtumiaji jambo litaondoa udanganyifu.

“Niwapongeze DART kwa kujibu hoja za wananchi, uzinduzi wa kadi janja na kuachana na matumizi ya karatasi unaleta mapinduzi makubwa ya namna  tunavyotaka kuwahudumia Watanzania katika usafiri wa Dar es Salaam, inakwenda kujibu hoja na kutatua  changamoto za wananchi za kulipa nauli,”amsema.

“Mimi nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kuhusu usafiri huu wa mwendokasi kuwa watu wanakaa vituoni muda mrefu kusubiria usafiri na nikiomba majibu kwa nini kuna changamoto hiyo naambiwa michakato inafanyika ni muda mrefu sasa barabara ya Mbagala imeisha na mabasi hakuna hivyo nawasihi angalieni suala hili kwa jicho la tatu,” amesema Waziri

Amesema uzinduzi huo unatokana na maendeleo ya teknolojia ya ukusanyaji wa nauli kwa DART,  ambayo inaufanya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kuwa katika kiwango cha juu kabisa.

Pia amewaagiza watu wa TEHAMA kuwa kadi hizo zinapatikana kwa urahisi na mfumo usilete shida kabisa na kuanza kulalamikiwa na wananchi wakati Rais Dk. Samia Suluhu ametoa fedha wakapatiwe mafunzo namna ya kuundesha .

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DART, Othmani Kihamia amebainisha mfumo huo unakwenda kuanza kutumika mara moja baada ya uzinduzi huo na utapunguza foleni , usumbufu wa chenji na matumizi ya karatasi .

Amesema mfumo wa kukusanya nauli wa kisasa wa kutumia kadi janja utasaidia kuepuka kutumia mfumo wa karatasi au keshi na kupunguza foleni.

“Kadi hizi zina ubora tofauti na zinazotumia maeneo mengine kwani zina vitu vingi ambavyo mtu anaweza kutumia sio kulipa tu nauli na mfumo  huu uliojengwa na Wakala hii  unafaida nyingi ikiwa kuondoa  matumizi ya karatasi yanayochangia uchafuzi wa mazingira,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here