Home KITAIFA RAIS DK.SAMIA:AMESISITIZA UMUHIMU WA HAKI, AMANI NA KUHESHIMIANA

RAIS DK.SAMIA:AMESISITIZA UMUHIMU WA HAKI, AMANI NA KUHESHIMIANA

Dar es Salaam

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa haki, amani, kuheshimiana, na kustahimiliana kama nguzo za kuimarisha umoja wetu kama taifa.

Hayo ameyasema leo Agosti, 31 2024 Dk. Samia wakati ameshiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’aan yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Tukio hili muhimu limeakisi dhamira ya Rais Samia ya kuendeleza umoja wa kitaifa na kudumisha amani katika nchi yetu.

Ameeleza kuwa mashindano haya yanachangia katika kuimarisha maadili ya kitaifa na kudumisha mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania bila kujali tofauti za kidini au kikabila.

“Naendelea kugusia umuhimu wa kuendeleza familia zetu na maadili ya nchi, akibainisha kuwa familia yenye misingi imara ni msingi wa taifa lenye nguvu. Amehimiza wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika mazingira ya heshima, amani, na upendo ili kuijenga jamii yenye maadili bora,”amesemaDk. Samia.

Pia amewekea mkazo juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii, alisema kuwa mwanamke ni mhimili wa familia na jamii kwa ujumla na aliwapongeza wanawake kwa kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto na kujenga maadili ya familia

Aidha Dk. Samia amekumbusha kuwa mtoto wa kiume naye asisahaulike katika malezi na miongozo ya maadili, kwani watoto wote wanapaswa kulelewa kwa usawa ili kuwa na jamii yenye uwiano.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha amani, mshikamano, na maadili mema ili kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha amani na mfano wa kuigwa duniani.

Mashindano haya ya Qur’aan yameleta pamoja washiriki kutoka mataifa mbalimbali, yakiwa ni jukwaa muhimu la kukuza maadili, uelewano, na mshikamano wa kimataifa. Rais Dk. Samia amewapongeza washiriki wote na kuwatakia kila la heri katika mashindano hayo, akisisitiza kuwa washindi ni wale wote waliohudhuria na kushiriki kwa dhati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here