Home KITAIFA RAIS DK.SAMIA KUSHIRIKI MKUTANO WA FOCAC NCHINI CHINA

RAIS DK.SAMIA KUSHIRIKI MKUTANO WA FOCAC NCHINI CHINA

Dar es Salaam

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa tisa wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika utakaofanyika Septemba 4 hadi 6, mwaka huu, jijini Beijing nchini China.

Akizungumza leo Agosti, 31 2024 jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema Rais Dk. Samia atashiriki mkutano huo kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.

Amesema mikutano hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubalishana kati ya China na nchi moja ya Afrika.

“Jukwaa la FOCAC lilianzishwa mwaka 2000 na Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika. Tangu kuanzishwa kwake jumla ya mikutano ya Kilele (Wakuu wa Nchi na Serikali) minane imefanyika,” amesema.

Amesema ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utaongozwa na Rais Dk. Samia ambaye ataungana na Wakuu wa Nchi na Serikali wenzake kutoka nchi zaidi ya 40 kati ya 54 za Bara la Afrika kushiriki mkutano huo.

Pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonia Guterres, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki watashiriki.

“Serikali ya China imemteua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC itakayofanyika Septemba 5, mwaka huuu akiiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki,” amesema.

Ameeleza kuwa mkutano huo wa utaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kushirikiana ili kuendeleza usasa na kujenga jamii bora ya China na Afrika kwa mustakabali wa pamoja’ ambayo inalenga kuwahamasisha viongozi wakuu wa nchi na serikali wa Afrika na China kujadili masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China kuongeza kasi ya maendeleo kwa pande zote mbili.

Amesema mkutano huo utagawanyika katika mikutano minne ya Ngazi ya Juu ambayo itafanyika kwa muda mmoja.

Balozi Kombo ametaja baadhi ya mada zitakazihadiliwa ni utawala wa nchi, mpango wa miundombinu na uwekezaji, maendeleo ya viwanda na kilimo cha kisasa na amani na usalama.

Amesem kila nchi inapaswa kuchagua mada moja ambayo itaijadili wakati wa mikutano hiyo ambapo kwa Tanzania itajikita katika mada ya maendeleo ya viwanda na kilimo cha Kisasa.

“Mada hii imezingatia Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano ambao ndiyo mpango wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025,” amesema.

Ameongeza kuwa akiwa nchini China Rais Dk. Samia atafanya mkutano wa uwili na Rais Xi Jinping, ambapo watajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo.

Pia baada ya mazungumzo hayo watashiriki hafla ya kutia saini Hati za Makubaliano kuhusu kuifufua Reli ya TAZARA.

Vilevile Rais Dk. Samia atafanya mikutano ya pembezoni mwa Mkutano wa Kilele wa FOCAC ambayo inalenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kuwavutia wawekezaji wa China kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

“Rais atafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuimarisha uhusiano uliopo Kati ya Bunge la Tanzania, Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Watu wa China,” amesema.

Pia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa na kufungua Ofisi zao nchini nchini na kukutana na kampuni kubwa za China kwa pamoja katika hafla ya chakula cha jioni yenye lengo la kuhamasisha kufanya uwekezaji nchini.

Balozi Kombo amesema kupitia mkutano huo Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali ikiwemo mipya na ile ambayo hajaweza kutelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kutekelezwa chini ya mpango kazi mwaka 2025-2027 kwa kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada.

Miradi hiyo ni ujenzi wa mtandao wa Mawasiliano Vijijini Awamu ya Pili, Ujenzi wa njia ya kusafirisha Umeme wa Kilovati 400 awamu ya pili na tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) awamu ya pili na ujenzi wa babara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.7

Mkutano huo una malengo makuu matatu ambayo ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China.Kujadiliana na kukubaliana na serikali ya China namna ya kuendelea kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele kwa maendeleo ya upande ya Taifa.

Vilevile kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili na kutangaza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya sera na sheria katika sekta ya biashara na uwekezaji kuvutia wawekezaji wengi kutoka nchini humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here