Home KITAIFA RC MTAMBI AWATAKA WANANCHI KUITUMIA HAIPPA PLC KUONDOA UMASIKINI

RC MTAMBI AWATAKA WANANCHI KUITUMIA HAIPPA PLC KUONDOA UMASIKINI

Na Shomari Binda-Musoma

MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewataka wananchi kujisajili na kujiunga na kampuni ya HAIPPA PLC ili kujikwamua kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa leo agosti 29 na mwakilishi wa mkuu wa mkoa Katibu Tawala Msaidizi mhandisi Mwita Okayo kwenye mkutano mkuu wa pill wa kampuni hiyo.

Amesema ajenda ya serikali ni kuondokana na umasikini ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa kampuni za uwezeshwaji wananchi kiuchumi.

Kanali Mtambi amesema Haippa PLC kupitia ubunifu inaoufanya ina malengo mazuri juu ya kuondoa umasikini na ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo.

Amesema ameifatilia HAIPPA PLC na wasimamizi wake na kuona inafaa na kusisitiza wananchi wengi kujiunga na kununua hisa ili kampuni hiyo iwe kubwa zaidi.

” Niko hapa kwa niaba ya mkuu wa mkoa ambaye yupo kikazi nje ya mkoa wa Mara kikazi lakini anaijua HAIPPA PLC na yuko pamoja nanyi.

” Kikubwa anasisitiza kununua hisa kwa wingi na kwa wale ambao bado hawajajiunga na HAIPPA PLC wafanye hivyo ili kuinuka pamoja,”amesema mwakilishi huyo.

Akitoa taarifa ya kampuni mkurugenzi wa HAIPPA PLC Boniphace Ndengo amesema chombo hicho kilianzishwa ikiwa na wawekezaji 8 walionunua hisa 3400 zenye thamani ya shilingi 1,700,000.

Amesema hadi kufikia desemba 31 2023 HAIPPA PLC ilikuwa na wanahisa 127 walioorodheshwa BRELA wakiwa wamejenga mtaji unaofikia shilingi 233,335,000 na wanaendelea kuujenga na hadi tarehe 28 agosti 2024 ulikuwa umefikia shilingi 273,440,000.

Mwenyekiti wa bodi ya HAIPPA PLC Bonamax Mbasa amesema kuanzishwa kwa kampuni hiyo haikuwa jambo rahisi na mafanikio makubwa yamepatikana.

Amesema hapo mwanzo kulikuwa na changamoto ya masoko kwa wakulima,wafugaji kwenye masoko kutokana na uonevu lakini baada ya ujio wa HAIPPA PLC imekua suruhisho.

Baadhi ya wanachama wa HAIPPA PLC wamesema wanajivunia kuwa wanahisa kwa kuwa kwa muda mfupi wameona mafanikio na kupata gawio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here