Home KITAIFA WIZARA YA MADINI, CHAMMATA WAKUTANA KUJADILI UTATUZI WA CHANGAMOTO

WIZARA YA MADINI, CHAMMATA WAKUTANA KUJADILI UTATUZI WA CHANGAMOTO

*Waziri Mavunde asisitiza marufuku Wafanyabiashara wa kigeni kufuata Madini Migodini

*Aelekeza Leseni za Biashara ya Madini kutolewa kikanda

*Wizara kuweka nguvu kwenye minada midogo ya ndani

*CHAMMATA wapongezwa kwa ushirikiano kudhibiti utoroshaji madini

Dar es Salaam,

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ameongoza kikao baina ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyabiashara wa Kati wa Madini – Broker (CHAMMATA) na kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na kuangalia namna ya kuzitatua kwa lengo la kuboresha shughuli zao zifanyike kwa ufanisi zaidi.

Kikao hicho kimefanyika leo Agosti 24, 2024, Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Dk. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga na baadhi ya Watendaji Wakuu wa Tume ya Madini pamoja na Uongozi wa CHAMMATA.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa CHAMMATA kuwa na anwani rasmi na kuwataka wafanyabiashara hao kutengeneza mfumo wa utambuzi unaozingatia sifa za “mabroka” na kwamba, Serikali iko tayari kuweka utaratibu wa kutambua wafanyabiashara hao wa kati kupitia CHAMMATA ili kuhakikisha ufanisi katika katika shughuli zao ikiwemo Serikali kuwafikia kwa urahisi.

“Baada ya kukamilisha masuala ya ofisi na utambuzi wa wanachama,Nitawapatia vifaa vya kuanzisha ofisi kama kompyuta na printer ili kuboresha shughuli zenu za kiofisi, muwe mnatambulika na kuwa na anwani na ofisi rasmi,” amesema Mavunde.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa Serikali imefungua milango kwa taasisi za fedha nchini kuona namna ya kushirikiana na Sekta ya Madini kwa kuwapa mikopo, akitolea mfano wa zaidi ya shilingi bilioni 10 zilizotolewa kwa wachimbaji mkoani Shinyanga hivi karibuni na kuwahimiza umuhimu wa kutunza kumbukumbu za uendeshaji wa shughuli za madini ili kuimarisha uaminifu kati ya wafanyabiashara na taasisi za fedha.

Aidha, Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Serikali itahakikisha Wafanyabiashara wa kigeni wanabaki kwenye masoko na hawaruhusiwi kwenda machimboni, kwani wao ni Wafanyabiashara wakubwa na siyo wa kati na kusisitiza kuwa, Serikali itafanya ukaguzi wa kina ili kuhakikisha jambo hilo halijirudii tena.

Vilevile, amemwelekeza Katibu Mkuu wa Madini kuweka utaratibu mzuri wa Leseni za Biashara ya madini kuwezesha wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao zaidi ya mkoa mmoja wakati Wizara ikiendelea kufanya maboresho kulingana na maombi na hoja zilizowasilishwa na chama hicho.

Awali, Mwenyekiti wa CHAMMATA, Jeremiah Kituyo aliwasilisha changamoto zinazowakabili na kuomba Wizara ya Madini kuwasaidia kutatua, ameeleza baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa madini, ikiwemo leseni kukatwa kimkoa, hali inayokwamisha ufanisi wa kazi.

Pia, Kituyo ameipongeza Serikali kwa kuratibu mashirikiano baina ya Taasisi za kifedha na Watu waliopo katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini na kutolea kuwa, hivi karibuni benki moja ilitoa mkopo wa shilingi milioni 300 kwa mabroka 25 mkoani Arusha, hatua ambayo ameitaja kuwa muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, Kipuyo ameishukuru Wizara kwa kuruhusu kufanyika kwa minada midogo ya Madini Mirerani na kueleza kwamba minada hiyo imesaidia kuifungua Mirerani kiuchumi na kutumia fursa hiyo kuiomba Wizara kuendelea kufanya hivyokwamadini mengine ya vito hususan almasi.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Madini Dk.Steven Kiruswa ameendelea kusisitiza chama hicho kuzingatia suala la kuwepo kwa mfumo maalum wa chama hicho na kushauri kuhusu umuhimu hicho kuweka utaratibu wa kukutana na Wizara mara kwa mara kujadili masuala yanayohusu biashara ya madini ya kwa lengo la kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara ya madini nchini.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema lengo la kikao hicho ni kutafuta suluhu ya matatizo yanayowasilishwa na wadau ili kuweka utulivu katika biashara ya madini kwa maendeleo ya sekta na kuongeza kwamba, ni utaratibu ambao Wizara imejiwekea wa kukutanana makundi mbalimbali ili kusikiliza na kutatua changamoto hatimaye Sekta ya Madini iendelee kuchangia ipasavyo kichumi na kimaendeleo kwa taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here