Home KITAIFA WAZIRI KOMBO APOKEA MWALIKO WA RAIS SAMIA KUSHIRIKI JUKWAA LA FOCAC

WAZIRI KOMBO APOKEA MWALIKO WA RAIS SAMIA KUSHIRIKI JUKWAA LA FOCAC

Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amepokea mwaliko rasmi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping utakaofanyika mwezi Septemba 2024 jijini Beijing nchini China.

Mwaliko huo umewasilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu China nchini Tanzania, Chen Mingjian katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, pia umeainisha nafasi ya kipekee kwa Dk. Samia Suluhu Hassan kuzungumza katika kikao cha ufunguzi kwa niaba ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na kuzungumza Katika Mkutano wa Ngazi ya Juu utakaojadili mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa.

Akipokea mwaliko huo kwa niaba ya Rais, Balozi Kombo ameelezea kuwa nafasi ya Rais kushiriki na kuzungumza katika Jukwaa hilo itaipa nchi fursa ya kuangazia uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, hali ambayo itasaidia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania ni kinara na kiongozi wa kupigiwa mfano kwenye Jumuiya hiyo kongwe Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here