Home KITAIFA TANZANIA INA MFUMO MZURI WA KUKABILIANA NA MAAFA KUANZIA NGAZI YA TAIFA...

TANZANIA INA MFUMO MZURI WA KUKABILIANA NA MAAFA KUANZIA NGAZI YA TAIFA HADI VIJIJINI.

Dar es Salaam

IMEELEZWA kuwa Tanzania ina mfumo mzuri wa kukabiliana na maafa kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini na kusisitizwa kuwa ikiwa itaendelea kusimamiwa vema changamoto nyingi zitafanyiwa kazi kwa haraka na ufasaha mkubwa.

Hayo yamebainishwa Agosti 19, 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali, Hosea Ndagala akimwakilisha, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga wakati wakilele cha maadhimisho ya Siku ya Huduma za Kibinadamu Duniani.

“Kabla ya kuingia hapa ukumbini nimepitia mabanda na nimeona maonesho ni dhahiri kwamba tuko tayari kukabiliana na majanga na maafa pindi yatakapojitokeza katika kutoa huduma za kibinadamu, pia kupitia maadhimisho haya tumejuana nani ni nani na ikitokea majanga tuanze na nani katika kukabiliana na maafa,” amesema.

Pia ametoa pongezi kwa RAPID -Tanzania na mashirika mengineyo yasio ya kiserikali kuitikia wito wa kushirikiana na Serikali na kuanzisha mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoyoshughulika na maafa na huduma za kibinadamu wakati wa majanga kwa kusaidiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu huduma na misaada ya kibinadamu ili iweze kufikia watu sahihi na kwa wakati sahihi.

Brigedia Jenerali Ndagala katika maadhimisho pia ametoa wito kwa mashirika mengine kujiunga na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanashughulika na maafa ili kuongeza ufanisi kwa kushirikiana na Serikali kujiandaa kwa maafa na kutoa huduma maafa yanapotokea.

Pia amewashukuru washirika na wadau wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa na Umoja wa Mataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo yameendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuiletea nchi maendeleo.

Amesema mchango wao umekuwa wa muhimu katika kuiwezesha nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.

Ameongeza kuwa nchi imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira.

Amesisitiza kuwa kutokana na changamoto hiyo Serikali imekuwa ikisimamia na kuratibu shughuli za kuzuia na kukabiliana na majanga kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa inayotekeleza majukumu yake chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Suala la Kuzuia na kukabiliana na majanga ni mtambuka ambalo linahitaji nguvu za pamoja katika kulishughulikia. Hivyo, leo suala hili linajidhihirisha wazi kwa kuona washiriki walioko hapa kutoka katika Idara mbalimbali, Taasisi za Serikali na Taasisi zisizo za kiserikali, wote ni wadau muhimu katika kushughulikia usimamizi wa maafa hapa nchini,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Rapid – Tanzania, Maria Bilia amesema kuwa licha ya kuwa wachanga kutokana na kuanzishwa mwaka 2021, wameweza kutoa elimu ya moto katika shule zipatozo 50 kwenye mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma.

Pia tukifanikiwa kupata msaada tutaweza kutoa mafunzo ya aina hiyo nchi nzima na kwa sasa wanatoa elimu hiyo kupitia wataalamu walipo katika taasisi hiyo kwa kujichangisha fedha ili kufanikisha mchakato huo ambao wanaamini umekuwa na tija katika kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo ya moto katika mashule.

Ameongeza kuwa maoni, ushauri uliotolewa na wadau katika njia za kukabiliana na majanga wameyapokea na wanakwenda kuyafanyia kazi ili kuongeza ufanisi katika jambo hilo kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Save the Children, Angela Kauleni , amesema wakati dunia ikiadhimisha siku hiyo, Tanzania kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la changamoto za kibinadamu zinayotokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uwepo wa wakambizi kutoka nchi jirani.

Amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi, zimeongeza mahitaji ya huduma za kibinadamu kwa kiwango kikubwa na kusababisha kuwepo kwa presha kubwa kwa watoaji huduma hizo na kusema kutokea kwa majanga ya mafuriko, tishio la kimbunga,maporomoko ya ardhi, milipuko ya magonjwa ya kuambukiza yamekuwa ni uhalisia wa mara kwa mara katika oparesheni zao za kukabiliana na dharura.

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Elkie Wisch ameweka wazi kuwa wakati dunia inaadhimisha siku hiyo ni vema nchi mbalimbali zikazingatia misingi ya sheria iliyowekwa kimataifa ili kusaidia kuwalinda watoa huduma za kijamii na kuwanusuru na vifo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here