Home KITAIFA TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA MAFUTA NA GESI MACHI 2025

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA MAFUTA NA GESI MACHI 2025

đź“ŚWadau Sekta ya Nishati zaidi ya 1000 kushiriki

đź“ŚDkt. Biteko awataka wadau kushirikiana kuelekea mkutano huo

đź“ŚNishati Safi ya kupikia kupewa kipaumbele

Na Mwandishi wetu

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameshiriki katika kikao cha maandalizi ya Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 5 hadi 7 Machi, 2025 katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku tatu wa kimataifa utafanyika chini ya kauli mbiu “Unlocking Investment in Future Energy: The Role of Petroleum Resources in the Energy Mix for Sustainable Development in East Africa” ambapo utatanguliwa na kufuatiwa na safari za kutembelea maeneo ya kijiolojia na kujionea vivutio mbalimbali kitalii vilivyopo katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Aidha, watazungumzia masuala ya mabadiliko kuelekea katika matumizi ya nishati safi na kuwakutanisha wadau zaidi ya 1000 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Biteko amesema “Kama nchi tumepata fursa ya kuandaa mkutano huu wa kimataifa na Serikali imepanga kufanya hivyo kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuandaa mkutano wenye tija kwa nchi na kutoa nafasi kwa Watanzania kufaidika na uwepo wa mkutano huu”.

Dk. Biteko ametoa rai kwa wahudhuriaji wa kikao hicho kutumia vema fursa ya uwepo wa mkutano wa EAPCE’25 kutangaza biashara, huduma na utaalamu wao pamoja na kujenga mitandao na washirika kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameeleza kuwa mkutano wa EAPCE’25 pia utahusisha maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali na hivyo kutoa fursa kwa wadau kuchangamkia fursa hiyo.

“Sambamba na mkutano na maonesho eneo lingine ambalo wadau wanakaribishwa kuchangamkia ni udhamini wa mkutano ambao unatoa nafasi ya kujitangaza ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia ukubwa wa mkutano wenyewe,” amesema Mhandisi Mramba.

Kikao hicho ni cha awali cha maandalizi kuelekea mkutano wa EAPCE’25. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti (www.eapce25.eac.int)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here