Home AFYA MOI YAADHIMISHA MIAKA 20 YA UPASUAJI WA NYONGA NA MAGOTI

MOI YAADHIMISHA MIAKA 20 YA UPASUAJI WA NYONGA NA MAGOTI

Dar es Salaam

TAASISI Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inaadhimisha miaka 20 ya mafanikio ya matibabu ya upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka kambi maalum ya upasuaji mpya na wa marudio wa viungo hivyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk. Lemeri Mchome amesema wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo Agosti, 19, 2024 kuwa miaka 20 ya matibabu ya kupandikiza nyonga na magoti bandia imekuwa ya mafanikio makubwa ambapo zaidi ya wagonjwa 5,000 wamepata matibabu yanayohusiana na nyonga au magoti.

Amesema Serikali imewekeza zaidi ya Bilioni 13.976 katika miundombinu, mitambo, vipandikizi na wataalam ambapo kwa wagonjwa hao waliotibiwa zaidi ya Bilioni 80 ziliokolewa kwa kuwatibia wagonjwa ndani ya nchi.

“Kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza, wataalam kutoka Marekani na Australia tumeandaa kambi hii maalum ya matibabu ya marudio ya upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti. (Revision Total Hip, Knee Replacement and megaprothesis Surgeries).

Pia madaktari watabadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji wa marudio na kuifanya MOI kuendelea kuwa kituo cha umahiri cha matibabu haya,” amesema Dk. Lemeri.

“Kambi hii inaenda sambamba na kuadhimisha miaka 20 ya utoaji wa matibabu hayo ya kibobevu; takriban wagonjwa 200 wanasubiria kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha nyonga au magoti na zaidi ya 58 wanasubiri upasuaji wa kurudia,”amefafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Mifupa MOI, Dk. Anthony Assey amesema katika kambi hiyo wagonjwa nane (8) wanatarajia kufanya upasuaji wa marudio na 12 upasuaji wa awali.

“Ndani ya miaka 20 ya utoaji wa matibabu ya kibingwa nakibobezi tumeweza kuzijengea uwezo hospitali za Bungando, Benjamini Mkapa, hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali Rufaa ya Kanda ya Kusini na tutaendelea kuwajengea uwezo katika mbinu hizi mpya,” amsema Dk. Assey

Naye Daktari Bingwa wa Mbobezi wa Nyonga na Magoti Dk. Greg William Stoacs kutoka nchini Marekani amesema ni furaha kwake kushiriki katika kambi hiyo ili kubadilishana uzoefu wa njia mpya za matibabu ya kubadilisha nyonga na magoti.
Kambi hii inahudhuriwa na madaktari bingwa kutoka Burundi, Uganda, Rwanda, Kenya, Ethiopia na Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here