Home AFYA RAIS SAMIA ALIPIA WASIOWEZA GHARAMA UPANDIKIZAJI FIGO

RAIS SAMIA ALIPIA WASIOWEZA GHARAMA UPANDIKIZAJI FIGO

Dar es Salaam

WAGONJWA wenye changamoto ya figo wanaohitaji kupandikizwa figo ambayo ni tiba stahiki kwa wagonjwa wanaosafisha damu na hawana uwezo wa kulipia gharama za upandikizaji watahudumiwa kupitia fedha alizotoa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ili ziweze kufanya kazi hiyo.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Profesa Mohamed Janabi wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wachangia viungo duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 13 Agosti na kuhudhuriwa na wananchi waliopandikizwa figo pamoja na wenzao waliowachangia figo.

Profesa Janabi amesema kwa sasa wanatafuta seti ya wagonjwa 10 na ndugu zao 10 ambao wapo tayari kuwachangia figo na watakapokidhi vigezo husika watanufaika na huduma hiyo.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tisa zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara zinazopandikiza figo Barani Afrika ambapo katika kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa huduma hiyo nchini, wagonjwa 102 wameishapandikizwa kupitia kampasi mbili za Upanga na Mloganzila.

Kwa upande wake mmoja wa wachangia figo, Juma Kanzaga ambaye alichangia figo akiwa na umri wa miaka 70, amewashukuru wataalam wote wa hospitali kwa kazi nzuri wanayofanya na kutoa wito kwa watanzania kuendelea kujitoa kuwachangia ndugu zao wenye uhitaji wa kupandikizwa figo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here