Home KITAIFA BRELA:WAKULIMA NI WADAU MUHIMU.

BRELA:WAKULIMA NI WADAU MUHIMU.

Na Esther Mnyika, Dodoma

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imesema wakulima ni wadau muhimu kwa sababu wanapozalisha mazao wanayaongezea thamani hivyo kuhitaji kusajiliwa nembo au alama za biashara.

Akizungumza leo Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma, Ofisa Usajili wa BRELA, Gabriel Girangay, amewashauri wakulima kusajili nembo na alama za biashara.

“Wakulima ni wadau muhimu kwa sababu wanazalisha bidhaa mbalimbali na kuzipeleka sokoni ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu watambue kwamba BRELA ni muhimu kwao katika kusimamia au kulinda bidhaa zao. Tutalinda vumbuzi zao katika masuala mbalimbali yanayohusiana na kilimo na teknolojia,” amesema Girangay.

Ameeleza kuwa BRELA inafanya kazi ya kusajili kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, kutoa leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kusajili viwanda vidogo na kulinda vumbuzi za wataalam mbalimbali.

“Tupo kwenye maonesho ya Nanenane kwa ajili ya kutoa elimu na huduma mbalimbali, ukifika katika banda letu utapata huduma za kusajiliwa jina la biashara na kila Mtanzania mwenye nia ya kuanzisha biashara afike kuna wataalam wa masuala ya Tehama, biashara, alama za biashara na huduma na shughuli zetu nyingi zinafanyika kidijitali,” amesema.

Ameongeza kuwa wanatoa leseni za biashara kundi A ambazo ni zile zenye sura ya kitaifa na kimataifa, wanaelimishwa kwanza na kama wanataka kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi au kutoa bidhaa kutoka nje na kuleta nchini watapata leseni BRELA.

Aidha amesema kama mtu anahitaji kupata taarifa yoyote kuhusu kampuni, majina ya biashara, leseni au wanaotaka kukopa na kuingia ubia wa kibiashara afike katika banda hilo au ofisi za wakala huo na atapatiwa.

Amesema BRELA inatoa leseni za viwanda vikubwa na vya kati vyenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 100 kwenda juu lakini Shilingi milioni 100 kwenda chini ni viwanda vidogo ambavyo pia wanavisajili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here