Na Benny Mwaipaja
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 24 wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za nchi za Afrika ambazo ni Wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) (Africa Caucus Meetings) unaofanyika katika Hoteli ya Transcorp Hilton, mjini Abuja Nchini Nigeria. Mkutano huo umefunguliwa rasmi tarehe 2 Agosti, 2024 na Makamu wa Rais wa Nigeria, Mhe Kashim Shettima.
Mkutano huo unajadili namna ya kuboresha biashara katika nchi za Afrika kwa kuweka mazingira mazuri ya kusisimua biashara kwa kujenga miundombinu itakayowezesha kukuza biashara miongoni mwa nchi za Afrika na wataweka msimamo wa pamoja na kupeleka agenda ya namna Taasisi za Fedha za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, zinatakiwa kuziwezesha nchi hizo kifedha na kiutaalam ili zifikie malengo husika.