Na. Benny Mwaipaja
BENKI ya Dunia imeipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika kutekeleza mradi wa kimkakati wa Reli ya Kisasa-SGR kwa kuwa ni miongoni mwa miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa mjini Abuja nchini Nigeria na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, Victoria Kwakwa, alipokutana na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Kando ya Mikutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Nchi za Afrika, ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia na Shiruka la Fedha la Kimataifa-IMF.
Dk. Victoria Kwakwa, amesema kuwa si rahisi kwa nchi nyingi za Afrika kujenga mradi mkubwa wa reli kama ilivyofanya Tanzania kwa kuwa ina gharama kubwa lakini kukamilika kwake kutachochea biashara katika eneo la Maziwa Makuu huku akimmwagia sifa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua rasmi safari za treni hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Kwa Upande wao, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dk. Natu El-maamry Mwamba, walipokea pongezi hizo kwa niaba ya Serikali na kueleza kuwa lengo la mradi huo ni kuunganisha baadhi ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki ili kufungua milango ya biashara.
Dk. Nchemba ametumia mazungumzo hayo kuzitaka Taasisi za Fedha za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, kuangalia uwezekano wa kuweka riba nafuu kwenye mikopo inayotolewa kupitia madirisha ya ujenzi wa miundombinu ili nchi za Afrika ziweze kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji hatua itakayochangia kukamilisha miradi husika kwa wakati.
Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania ambapo imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika miradi mbalimbali ya kimkakati ya maendeleo pamoja na kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali.