Na Benny Mwaipaja, Abuja
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba akiwa na Ujumbe wa Tanzania katika Ubalozi wa Tanzania, uliopo Abuja nchini Nigeria, ambapo yeye na ujumbe wake, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dk. Natu El-maamry Mwamba na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango-Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi, wanashiriki Mikutano ya Nchi za Afrika (African Caucus Meetings), ukiwashirikisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Dk. Nchemba na ujumbe wake walipowasili katika Ubalozi huo, walilakiwa na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Judica Nagunwa akiambatana na Mwambata Jeshi wa Ubalozi Brigedia Jenerali Julius Kadawi na Maafisa wengine waandamizi.
Akizungumza na Watumishi wa Ubalozi, Dk. Nchemba, aliupongeza Ubalozi huo kwa kusimamia vema Diplomasia ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka katika Taifa hilo kubwa barani Afrika.
Ametoa wito kwa Ubalozi huo kufanya utafiti namna lugha ya kiswahili inaweza kunadiwa katika Mataifa kadhaa ya kiafrika wanayoyasimamia kutokana na umuhimu wa lugha hiyo katika kuunganisha Bara hilo.
Amesema kuwa kiswahili ni bidhaa ambayo ikienea na kutumiwa na Mataifa mengi duniani itakuza ajira kwa walimu wa kitanzania watakaotumika kufundisha lugha hiyo lakini pia kuharakisha maendeleo katika nchi zitakazozungumza lugha hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Judica Nagunwa, amesema watalifanyia kazi suala la kukuza matumizi ya kiswahili katika nchi wanazoiwakilisha nchi na kwamba tayari kuna Ushirikiano na makubaliano ya kitaasisi kati ya Tanzania na Nigeria katika kueneza lugha ya kiswahili kupitia vyuo vikuu vya Tanzania na Nigeria lakini pia kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Aidha, Nagunwa amesema kuwa Nigeria ni nchi kubwa kiuchumi na kwamba Tanzania imenufaika na uwekezaji wake nchini Tanzania, kikiwemo Kiwanda cha Saruji cha Dangote na Benki ya UBA.