Dar es Salaam
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amesema ufadhili uliotolewa na Serikali ya Uswisi kusaidia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), umesaidia kukuza na kuimarisha kazi ya sekta hiyo nchini.
Amebainisha hayo Julai 26, 2024 jijini Dar Es Salaam, wakati akizungumza na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania aliyemaliza muda wake Didier Chassot.
“Kwa mujibu wa kanzidata yetu, kuanzia Julai 2023 hadi Julai 2024 jumla ya mashirika 24 yamepokea msaada wa ufadhili kutoka kwa Serikali ya Uswisi na kufikia shilingi Bilioni 23.3.
Ni msaada mkubwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa vijana na wanawake kiuchumi, afya na kusaidia Asasi za Kiraia.” amesema Dk. Gwajima.
Dk. Gwajima amesema kiasi hicho sio tu kwamba kimesaidia NGOs lakini pia imebadilisha maisha ya wanawake na vijana wengi katika jamii.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa Msaada wa kiufundi wa shilingi Milioni 200 kwa ajili ya uboreshaji wa mfumo wa usajili wa NGOs (NIS) na uboreshaji wa ramani ya kidijitali inayowezesha Jamii kupata moja kwa moja taarifa za NGOs, kutazama shughuli na miradi yao kwa maeneo na afua wanazotekeleza na kutoa nafasi kwa wadau wa Maendeleo kushiriki fursa inayopatikana ambapo takribani NGOs 10,330 zinapatikana kwenye mfumo huo.
Ameongeza kuwaWizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ndiyo kitovu cha ubora katika kukuza maendeleo ya jamii, usawa wa kijinsia, ustawi wa jamii na haki za watoto kupitia sera, mikakati na miongozo, hivyo kushirikiana na wadau wengi zaidi nchini ni muhimu ili kufikia matokeo yanayotarajiwa.
Naye Balozi Chassot ameishukuru Serikali ya Tanzania katika nyanja zote hasa ushirikiano mzuri uliopo baina nchi hizi mbili.
Amempongeza pia Waziri Dk. Gwajima kwa utendaji wake akiwa ni wa kwanza wa wizara hiyo na kusema amefurahia uwepo wake nchini na nafasi yake katika kuwezesha masuala ya Jinsia na NGOs kupitia Wizara hiyo.