Home KITAIFA BoT IMESEMA INAWAJIBU WA KUIKOPESHA SERIKALI MKOPO WA MUDA MFUPI USIO...

BoT IMESEMA INAWAJIBU WA KUIKOPESHA SERIKALI MKOPO WA MUDA MFUPI USIO WA KIBAJETI WA ASILIMIA 18.

Dar es Salaam

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema inawajibu wa kuikopesha serikali mkopo wa muda mfupi usio wa kibajeti wa asilimia 18 ambapo sheria ya mwaka 2006 sura ya 197 imewapa uwezo wa kuikopesha mkopo huo ili iweze kuziba mapengo ya muda mfupi na si kufadhili bajeti.

Pia amesema sheria hiyo ya kukopesha serikali mkopo wa muda mfupi ipo kwa benki kuu nyingi duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22,2024 Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki BoT, Agathon Kipandula amesema kuwa mkopo unaotoa kwa serikali upo kwa mujibu wa sheria sura ya 197 ya mwaka 2006.

Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, benki hiyo inatunza fedha za serikali zote mbili na mashirika ya umma hivyo, pale wanapokuwa na uhitaji huwakopesha.

‘’Sheria hii pia imeweka ukomo wa kukopa ambao kwa mujibu wa sheria ni asilimia 18 ya mapato ya mwaka jana,’’ amefafanua Kipandula.

Ameeleza kuwa kwa sababu ya kuwa na mteja ambaye ni serikali, sheria hiyo imetoa nafasi ya kutoa mkopo wa muda mfupi kwa lengo la kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya serikali.

Kipandula amesema kuwa utaratibu huo unaofanyika kwa benki kuu zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani kwani wote wanatumia sheria moja.

‘’Kwa mambo ambayo yanaendelea, sheria inatusimamia katika kuendesha shughuli za serikali ikiwemo kutoa huduma ya mkopo wa muda mfupi kuziba pengo au nakisi,’’ameongeza.

Aidha Kipandula amesema sheria hiyo inaitaka serikali kuchukua mkopo huo usio wa bajeti, ndani ya siku 180 na kwamba kila mwisho wa mwezi serikali inarudi katika nafasi yake na kurejesha mkopo huo.

‘’Mkopo huu sio ule ambao tunadetermine amount kwamba watakopa kiasi hiki, huu unabalance cash flow yake kwamba kama leo anajukumu la kulipa Sh 10,000 na alizo nazo ni Sh 5,000 basi Sh 10,000 itakuja kama overdraft na akipata fedha zake basi atarudisha,’’amesema.

Amesisitiza kuwa si kweli kwamba serikali ilikopeshwa kiasi cha fedha na BoT kwa aina tofauti kwani hata kwenye vitabu vya serikali hakuna kiasi hicho.

Aidha, amesema kuwa mkopo wa aina hiyo hauhitaji kupitishwa na bunge isipokuwa wataonesha kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).

‘’Kulikuwa na taarifa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Fedha ameshalitolea ufafanuzi, tunachokieleza hapa ni kuongeza uelewa wa masuala yanayoendelea kufanywa na BOT,’’ amefafanua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here