Home KITAIFA WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA NA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA

WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA NA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA

*ujenzi wa barabara za Chamwino umezingatia Waterbeach kwa mguu na wanaofanya mazoezi

Na Catherine Sungura, Chamwino

MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amewaomba wananchi kutunza na kulinda miundombinu ya barabara ikiwemo taa za barabarani.

Mhandisi Seff ametoa wito huo leo Julai 19 2024 wakati wa ukaguzi wa barabara zilizojengwa na TARURA kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ‘Ecoroads’ wilayani Chamwino.

‘Serikali imewekeza fedha nyingi kwa kujenga miundombinu hii hivyo wananchi wanao wajibu wa kusaidia katika utunzaji na kulinda miundombinu ya barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu,”amesema

Amesema wapo baadhi ya wananchi wanaiba betri za taa za barabarani hivyo ni wajibu wao kuzilinda na kuzitunza taa hizo kwa manufaa ya maeneo yao.

Hata hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwenye ofisi za Wakala huo mahali popote wanapoona sehemu ya barabara ina changamoto au inahitaji matengenezo ya haraka ili wafike kutengeneza.

Aidha, Mhandisi Seff amesema kuwa ujenzi wa barabara za Chamwino umezingatia Usalama wa watumiaji wa aina zote wa barabara hususani watembea kwa miguu hivyo amewataka wananchi wanaotembea kwa miguu na wale wanaofanya mazoezi kutumia njia za pembeni za watembea kwa miguu ‘walkways’ ili kuepuka ajali za barabarani na kujenga afya zao.

Naye, Rehema Mahajili mkazi wa Chamwino mtaa wa Umoja amesema wanafurahi kuona barabara zinabadilika ambapo imewasaidia kuboresha usafiri hususani kuzifikia huduma za afya na kuwaepusha kutembea kwenye vumbi kwakuwa barabara sasa hivi zimekuwa nzuri.

Barabara za Chamwino zenye urefu wa kilometa 6.95 zimejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuboresha udongo kabla ya kuweka lami juu ijulikanayo kama ‘Ecoroads’ ambapo teknolojia hiyo imetumika kujenga barabara katika wilaya ya Mufindi, Rufiji pamoja na Dodoma mjini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here