Katavi
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, amesisitiza kwa wakulima kulinda maeneo ya kilimo ili miradi ya skimu za umwagiliaji zinazoletwa zisaidie wakulima. Msiuze ardhi kiholela ili mnufaike na miundombinu inayojengwa.
Pia ameongeza kuwa wakulima wazingatie utunzaji wa miundombinu ya umwagiliaji kufuatia mafunzo waliyopatiwa Julai 19 2024 kuhusu Sheria, Kanuni na taratibu za uendelezaji wa miradi hiyo.
Tume ya Umwagiliaji pia inajenga maghala mawili; moja kwa akili ya kuhifadhi mpunga na mchele; na kingine kwa ajili ya kuwekwa mashine ya kukobolea mpunga.
Aidha, Waziri Bashe ameilekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha kuwa inajenga nyumba kwa Maafisa Ugani wa Kata husika; na kujenga mifereji ya maji na barabara.
Imeelezwa kuwa, katika Mkoa wa Katavi eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 124,761; ambapo kuna skimu za umwagiliaji 15 zimeshasajiliwa; miradi 12 inafanyiwa upembuzi yakinifu. Aidha, miradi 2 ipo katika eneo la Kamage na Mwamkulu kwa gharama za zaidi ya Shilingi Bilioni 50; ambapo hadi sasa asilimia 22 za ukarabati umefanyika.
Miradi hiyo ni hekta 2,500 eneo la Kabage; na hekta 3,000 eneo la Mwamkulu. “Litakuwa jambo la kusikitisha endapo miundombinu itakuwa inaharibiwa. Tulinde miundombinu kwa kuchangia mfuko wa maendeleo ya umwagiliaji ili ule mfuko usaidie kukarabati marekebisho yatayojitokeza katika skimu za umwagiliaji na miundombinu yake,” amesisitiza Waziri Bashe.