Home KITAIFA ANASWA AKITENGENEZA DAWA FEKI ZA KULEVYA

ANASWA AKITENGENEZA DAWA FEKI ZA KULEVYA

Dar es salaam

SHABANI Musa Adam mwenye umri wa miaka 54 anashikiliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ( DCEA) kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya zinazojulikana kama heroin kwa kutumia dawa tiba asili zenye asili ya kulevya akichanganya na kemikali bashirifu.

Akizungumza leo Julai, 17,2024 Jijini Dar es salaam Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa nyumbani kwake Manzese Kilimani Juni 11,2024 na baada ya kuhojiwa ameieleza kuwa siku za nyuma alikuwa akitengeneza dawa hizo katika nchi za bara la Asia kwenye magenge ya wazalishaji wa dawa za kulevya na pia alitumika kama mbebaji wa bidhaa hiyo (Punda) na aliporeje nchini aliendelea na uhalifu

Mamlaka inamshikilia mtu mwingine mmoja aliyetambulika kwa jina la Mbaba Rabini Issa Mtanzania mwenye pasipoti namba TAE442718B ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melchior Ndadaye Bujumbura Burundi akiwa na kiasi cha kilogramu 3.8 za skanka ambapo dawa hizo alikuwa amezificha kwa kushonea ndani ya begi la nguo na alikutwa akijiandaa kusafiri kuelekea Dubai.

“Ukamataji wetu unaendana kufuatia mikataba ya kikanda na kimataifa iliyosainiwa na Tanzania katika Udhibiti wa dawa za kulevya hivyo mhalifu yeyote wa dawa za kulevya atakayefanya uhalifu katika nchi zilizoingia makubaliano na kukimbilia moja ya nchi hizo atakamatwa na kuchunguzwa na akikutwa na kosa atawajibishwa kisheria,”amesema Kamishna.

Kamishna Lyimo amesema Mamlaka imeshakamilisha kanzi data (Data base) ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya na imeanza uchunguzi juu ya watu hao na wengi wamebainika wapo ndani ya nchi na wengine nje ya nchi baadhi yao wana biashara nyingine halali lakini wanajihusisha na biashara za kulevya na kufanya utakatishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Mhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo inahudumia walioathirika kwa dawa za kulevya na waliopo kwenye kanzi data yao ni takribani watu 3840 na kwa siku watu 900 wanaenda kunywa methadone na wengi wao wana matatizo ya kuathirika mapafu figo na moyo.

Amesema matumizi ya dawa za kulevya huathiri mfumo wa umeme wa moyo na kusababisha vifo vya ghafla.

Aidha Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya inathamini na kutambua ushirikiano unaotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wale wanaoelemisha juu ya athari za utumiaji dawa za kulevya , ikiwemo asasi vyombo vya habari pia Hospitali ya Taifa ya Mhimbili kwa kutoa tiba hivyo wametoa tuzo ili kama zawadi ili waendelee na mapambano hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here