Na Esther Mnyika,Dar es Salaam
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Yusuph Mwenda amesema kila wiki viongozi wa mkoa wa Mamlaka hiyo kukaa na wafanyabiashara ili kusikiliza changamoto zao za kikodi ili waweze kutatua kwasababu ndio wadau wao.
Pia amesema utekelezaji wa maagizo yaliyowekwa na Serikali wakati wa kikao cha wadau cha kujadili na kutafuta suluhisho la mgogoro wa wafanyabiashara unaendelea vizuri na tayari hatua kadhaa zimechukuliwa.
Hayo ameyasema Julai 15, 2024, Mwenda kuhusu hatua iliyofikiwa wa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo kusitisha kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za mashine za kielektoniki (EFD), kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi.
“Kuweka mfumo wa utoaji nyaraka za manunuzi wakati wa uagizaji bidhaa, kubainisha na kusimamia orodha ya bidhaa nane kuwa na bei elekezi, kukamilisha maboresho ya mfumo wa Tancis na wataalamu wa forodha kukutana na Jumuiya za wafanyabiashara nchini ili kujadiliana taratibu za kiforodha,”amesema.
Amesema mpaka sasa wamekamilisha utengenezaji wa mifumo miwili ikiwemo wa kutoa nyaraka za manunuzi na bei elekezi eneo la forodha hivyo mifumo hiyo ikianza hawatarajii kupata malalamiko kutoka kwa walipakodi.
Ameeleza kuwa TRA imejipanga kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa walipakodi na umma kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina za mabadiliko ya sheria za kodi zinazogawa aina za walipakodi mfano Wauzaji wa Vitenge na wauzaji wa vito vya thamani.
Amesema mfumo wa kuruhusu kutoa nyaraka za manunuzi umekamilika tangu Julai 3, mwaka huu hivyo wafungashaji bidhaa (consolidator) kila mfanyabiashara atapata taarifa za kiforodha pia ataweza kulipa kodi moja kwa moja bila kupitia kwa mfungashaji na kwamba ataelewa ni kodi gani imelipwa.
Mwebda amesema kukamilika kwa Mfumo huo kutasaidia kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata nyaraka zake za kiforodha na pia ataweza kulipia kodi moja kwa moja bila ya kupitia kwa mfungashaji wa mizigo yaani (Consolidator).
Amesema, katika suala la Kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo ni vitenge,Mashati,nguo nyingine,vipodozi,Vito vya thamani,nguo za ndani,leso na vesti zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika magari kazi hiyo tayari imeshafanyika na orodha ya bidhaa hizo nane tayari zimeshawekwa kwenye Tovuti ya TRA zikionyesha aina ya bidhaa, aina ya malighafi, vipimo vyake, bei ya bidhaa na kodi ya bidhaa husika.
Mwenda amesema maboresho ya TANCIS yakijumuisha mfumo wa Auto valuation yanaendelea kwa sasa yapo kwenye hatua za utengenezaji wa mfumo na Maboresho hayo yatakamilika kufikia mwezi Januari, 2025 kama ilivyoelekezwa na Serikali.
“Hadi sasa kampuni 16 za Wafungishaji mizigo (Consolidators) wanaoagiza bidhaa tayari wameshapewa mafunzo kwa ajili ya kuanza kutumia mfumo huo na zoezi hilo limeambatana na kutoa elimu na uwezo wa kutumia mfumo huo,”amesema
Aidha Mwenda amesema TRA ilitekeleza agizo la taratibu za kiforodha hususani uthaminishaji na ugomboaji wa mizigo Julai3 mwaka huu kwani Kamishna wa Forodha aliitisha kikao cha majadiliano na viongozi wa Jumuiya za Wafanyabiashara Tanzania ambao waliwakirishwa na Viongozi wao 11.
“Katika kikao hicho, baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na mfumo wa ufungishaji mizigo unavyofanya kazi na kujadili bei elekezi za bidhaa nane ambapo TRA inaendelea kutoa elimu kwa walipakodi na kufanya mapitio ya viwango vya kodi,”amesema.
Amesema ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari kulingana na thamani ya biashara zao ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zote za wafanyabaishara zilizowasilishwa Serikalini hususani zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria,”Amesema Mwenda.