Home KITAIFA TANESCO KUANZA KUFANYA MABORESHO YA LUKU MKOA WA PWANI NA DAR ES...

TANESCO KUANZA KUFANYA MABORESHO YA LUKU MKOA WA PWANI NA DAR ES SALAAM


Dar es salaam

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kutakuwa na maboresho huduma zake katika mfumo wa Luku kwa wateja wake wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kuanza Julai 22, 2024 ili kuendana na mabadiliko ya mfumo wa mita za luku ya Kimataifa na kuongeza ufanisi na usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 15,2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma TANESCO, Irene Gowelle, amesema maboresho hayo yatakuwa pale ambapo mteja atakaponunua umeme kwa mara ya kwanza na kupokea tarakimu kwenye makundi matatu na kila kundi litakuwa na tarakimu 20.

Ameongeza kuwa kundi la kwanza na pili la tarakimu litakuwa kwa ajili ya maboresho ya mfumo wa luku, huku kundi la tatu kwa ajili ya umeme utakaokuwa umenunuliwa na mteja.

“Mteja ataingiza umeme tarakimu za kila kundi katika luku yake kwa mfatano unaosomeka kwenye risiti ya malipo au ujumbe mfupi wa maandishi (sms) na kila utakapoingiza kundi moja mteja anapaswa kubonyeza alama ya kukubali ya # au msale wa kukubali na hapo utakuwa umefanikiwa kuboresha mita yako na kupokea kiwango cha umeme ulionunua,” amesema Gowelle.

Pia wateja ambao watashindwa kufanya maboresho ya luku mpaka kufikia Novemba 24, 2024 watakosa huduma ya umme hadi wakapofika katika ofisi za TANESCO kwa ajili ya kupata msaada wa maboresho ya mfumo wa luku.

Amesema kuwa TANESCO wajipanga katika mikoa yote kwa ajili ya kuwasaidia wateja wakati wanapopata na changamoto katika kipindi chote cha maboresho ya mita za luku.

“Zoezi la maboresho ya luku ni bure na litafanyika mara moja kwa kila mteja na baada ya kufanya hivyo atakuwa amefanya maboresho na ataendelea kupata kundi moja la tarakimu 20 kila atakapofanya manunuzi ya umeme,” amesema Gowelle.

Amesema kuwa baada ya mikoa ya Kusini na Kanda ya Nyanda za juu kusini zoezi kukamilika, litaendelea kwa mikoa mingine nchini kwa awamu kadri Shirika la TANESCO litakavyotangaza kwa umma, huku na mwisho wa zoezi hilo nchini ni Novemba 24, 2024.

Aidha endapo mteja atakutana na changamoto wakati anafanya maboresho ya mita za luku atawasiliana na Mkoa husika wa Kitanesco kupita namba : Mkoa wa TANESCO Temeke – 0694 169 798, Ilala – 0733 212 575, Kinondoni Kusini – 0756 251 753, Kinondoni Kaskazini – 0692 7685 87, Pwani – 0738 256 237 ambapo kampeni ya maboresho ya mita za Luku imebeba kauli mbiu inayosema ‘Mita yako tunakazi nayo’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here