Dar es Salaam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka Wizara na Taasisi zinazohusika na biashara na uwekezaji katika Serikali ya Zanzibar na Jamhuri Muungano wa Tanzania, kuondoa urasimu na tozo kwenye maeneo ya kimkakati pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara.
Ameyasema hayo leo Julai 13, 2024 wakati akifunga maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam (DTIF) na kuongeza kuwa Serikali hizo zina nia thabit ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Amesema maonesho hayo ya kimataifa yenye kaulimbiu ya “Tanzania ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji” yanakwenda sambamba na azma ya serikali ya kufungua nchi katika masoko pamoja na kuvutia uwekezaji.
“Nitoe wito kwa taasisi zetu zinazosimamia biashara na uwekezaji kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kuondoa urasimu na kuwezesha biashara zaidi, tunalenga kurahisisha biashara katika maeneo ya kimkakati ili kuchangia pato la Taifa na pato la mwananchi mmoja mmoja,” amesema Dk. Mwinyi.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo amesema maonesho hayo yametoa fursa ya elimu kwa Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi ambapo pia yaketoa fursa ya masoko.
Amesema Tanzania ni sehemu salama ya kufanya biashara na uwekezaji ambapo amewaalika Wafanyabiashara kufanya uwekezaji nchini.
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaban amewakaribisha Wafanyabiashara katika maonesho ya utalii na uwekezaji yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26 mwaka huu mjini Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade ), Latifa Hamis amesema jumla ya taasisi na watu binafsi 3,886 wameshiriki katika maonesho hayo ambayo kwa mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa ikiwepo kufungua masoko na mahusiano kwa Wafanyabiashara wa nchi mbalimbali