Home KITAIFA KAMATI GEF YATAKA USHIRIKIANO KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE

KAMATI GEF YATAKA USHIRIKIANO KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE

Dodoma

MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na Kamati yake ili kutatua kero zinazowakabili wanawake katika masuala ya kisheria.

Ameyasema hayo jijini Dodoma Julai 11, 2024 wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwenye Wizara ya Katiba na Sheria yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa Wizarani hapo.

Pia amesisitiza Wizara ya Katiba na Sheria kutupia jicho kwa makundi maalum wakiwemo wanawake hususani maeneo ya vizuizi ikiwemo mahabusu na magereza ili kuwasaidia wasiokuwa na uwezo wa kupata msaada wa kisheria.

“Lakini pia mnapotekeleza kampeni hii ya msaada wa kisheria pia kamati hii ipate ripoti ili kuona ni namna gani tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na kufikia azma ya Rais wetu ya kuwa na kizazi chenye usawa bila kumwacha mtu nyuma,” amesema Kairuki.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Mbaraka Stambuli, amesema tabia ya watu kutokuwa na utaratibu wa kuandika wosia wa mali zao wakiwahai imekuwa ndiyo chanzo cha ongezekoa la migogoro kwa familia hasa kwenye mgawanyo wa mirathi.

Aidha amesema, kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria inayotekelezwa na Wizara hiyo inayojulikana kama Mama Samia Legal Aids, katika mikoa saba ambayo wameshatoa huduma ya kutatua migogoro mbalimbali huku migogoro iliyoongoza ni mirathi pamoja na ardhi.

“Kuandika mirathi kutasaidia ndugu, watoto pamoja na jamaa wa karibu wenye maslahi na mali hizo kuondokana na migogoro na usumbufu wowote unaweza kujitokeza mara baada ya mmiliki kufariki” amesema Stambuli

Wakati huo huo Kamati hiyo imekutana na kuzunguza na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Jijini Dodoma ikilenga kupata maoni ushauri na changamoto zilinazowakabili Wanawake katika kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya Wajumbe wa Jukwaa hilo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo upatikanaji wa mikopo na fursa za masoko ya Ndani na nje ya Nchi.

Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Rais kuhusu Kizazi chenye Usawa inaendelea na ziara yake Mkoani Dodoma iliyojikita katika kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa Programu hiyo katika Makundi mbalimbali ikiwemo Taasisi za Serikali, Majukwaa ya Uwezeshaji kiuchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here