Home KITAIFA GAVANA BoT AISHUKURU IMF KWA MCHANGO WAKE KUENDELEZA UCHUMI TANZANIA

GAVANA BoT AISHUKURU IMF KWA MCHANGO WAKE KUENDELEZA UCHUMI TANZANIA

Dar es Salaam

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa mchango wake katika kuendeleza uchumi wa Tanzania hususani kipindi hiki ambacho dunia imekumbwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi.

Gavana Tutuba ameyasema hayo alipokutana na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya kanda ya Afrika ya IMF, Catherine Pattillo Julai, 112024 katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu, jijini Dar es Salaam. 

‘’Ningependa kuwashukuru IMF kwa mchango wenu katika maendeleo ya Tanzania kupitia utoaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi, mafunzo pamoja na ushauri mnaotupa kupitia mipango ya Extended Credit Facility (ECF) na ule wa Resilient and Sustainable Fund (RSF),” amesema Gavana Tutuba. 

Ameongeza kuwa Benki Kuu ya Tanzania imenufaika na mafunzo kutoka IMF ambayo yameisaidia BoT kuhamia kwenye mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba tangu Januari 2024. 

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa IMF, Pattillo, ameipongeza Benki Kuu na Serikali kwa ujumla kwa kutekeleza vizuri mpango wa ECF ambao unahusisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi na ule wa RSF katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizopo duniani kwa sasa. 

Pia, ameipongeza BoT kwa kufanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kupitia ufanisi katika utekelezaji wa sera ya fedha.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.1, na unatarajiwa kubaki chini ya asilimia 5 kwa mwaka mzima wa 2024. Maoteo haya yanategemea uwepo wa chakula cha kutosha nchini na sera thabiti za kifedha na kibajeti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here