Home KITAIFA DK.JAFO:WMA YAAGIZWA KUANZA KUPIMA MITA ZA UMEME NA DIRA ZA MAJI KABLA...

DK.JAFO:WMA YAAGIZWA KUANZA KUPIMA MITA ZA UMEME NA DIRA ZA MAJI KABLA HAZIJAFUNGWA

Pwani

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo ameiagiza Wakala wa Vipimo (WMA) kukamilisha utaratibu wa kupima mita za umeme na dira za maji kabla hazIjafungwa kwa wateja ndani ya mwezi mmoja ili kulinda haki za walaji.

Dk. Jafo ameyasema hayo Julai 11, 2024 alipotembelea WMA katika Kituo cha uhakiki wa vipimo Misugusugu Mkoani Pwani akiwa ameambata na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyonBalozi Dk.John Simbachawene pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Wizara, Sempeho Manongi.

Akiwa katika ziara hiyo yenye lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu shughuli zinazotekelezwa na WMA , Dk.Jafo ameiekekeza wakala hiyo kuwalinda wakulima wa mazao mbalimbali kuuza mazao yao kama vile pamba katika vipimo sahihi hususani kwa kudhibiti lumbesa ili wapate haki yao sawasawa na ujazo sahihi wa mazao yao.

Vilevile ametoa wito kwa wazalishaji saruji pamoja na vifaa vingine vya ujenzi kuhakikisha kuwa vinakuwa katika vipimo sahihi kulingana na ujazo uliotajwa ili kuwalinda wafanyabiashara na walaji wa bidhaa hizo kwa kupata bidhaa zinazolingana na thamani yake.

Aidha, ametoa wito kwa watumishi wa wakala hiyo kuendelea kufanya kazi kwa upendo na ushirikiano na kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora na kwa wakati kwa wafanyabiashara na kuwalinda walaji kwa kuhakikisha wanapata bidhaa katika vipimo sahihi kulingana na gharama yake ili kuleta usawa baina ya mtoa huduma na mlaji.

” Suala la vipimo ni Ibada hata vitabu vyote vya dini vimeeleza kuwa kila bidhaa inayouzwa iwe katika vipimo sahihi bila kumhujumu mlaji. Hivyo WMA tuwahamasishe wananchi hususani wakulima watumie vipimo sahihi wanapouza au kununua bidhaa ili wapate haki yao wanaostahili,” amesisitiza Dk. Jafo.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla amesema WMA imepoka maelekezo yote yaliyotolea na kuahidi kuyafanyia kazi katika muda uliopangwa kupitia Ofisi zake katika mikoa yote Tanzania bara na katika mipaka yote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here