Dar es Salaam
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) limewataka wananchi kuhakikisha kila mita wanayoitumia ikiwemo ya maji na umeme ziwe zimefanyiwa uhakiki kabla ya kuiingiza katika matumizi ili waweze kufanya malipo sahihi ya fedha yanayoendana na matumizi yao.
Wito huo umetolewa Julai 4, 2024, wakati wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo, Meneja wa WMA Mkoa wa Iringa, Lina Msuya, amesema ni muhimu mwananchi yoyote kuhakikish anatumia mita yenye nembo ya WMA ili kuepuka kuingia gharama zisizoendana na matumizi yake.
“Mita za maji na umeme ambazo ni mpya kabla mteja hajafungiwa mamlaka husika wanazileta kwetu kwaajili ya kufanyiwa uhakiki, na ambayo itakutwa iko vizuri inawekwa nembo ya WMA inayoonyesha kwama kifaa hicho kiko tayari kwa matumizi,” amesema.
Aidha amesema kuwa jitihada hizo zinafanyika kwa dhima ya kuhakikisha kwamba wanamlinda mlaji ili awe analipa bili ya maji au umeme inayoendana na matumizi yake halisiå.
Ameeleza kuwa wanatoa elimu kuhusiana na vifaa vinavyotumika kwaajili ya kupima mita ambazo tayari ziko katika matumizi ili kumfanya mwananchi awe na uelewa kwa uwanda mpana juu uya suala hilo.
Amesema kwa mwananchi ambaye tayari ameshafungiwa mita lakini akahisi kwamba bili anayoletewa ni kubwa kuliko matumizi yake aandike barua kwa wakala wa vipimo au apige simu bure kwa namba 0800 110097.
“Lakini kwa yule ambaye hjafungiwa bado basi ahakikishe mita atakayofungiwa iwe imehakikiwa na wakala wa vipimo kwa maana kwamba lazima iwe na nembo ya WMA, na ile ambayo haijahakikiwa na tayari iko kwenye matumizi itafanyiwa uhakiki kwa gharama za mamlaka zinazohusika,” amesema Lina