Home KITAIFA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YALIPONGEZA SHIRIKA LA KIVULINI.

SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YALIPONGEZA SHIRIKA LA KIVULINI.

Mwanza

KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah amepongeza mchango wa Shirika la KIVULINI katika kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii

Ametoa pongezi hizo Julai 4, 2024 akiwa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kwenye ziara ya kimafunzo ya kujifunza mbinu za kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ya mbinu ya SASA iliyoonyesha mafanikio katika kampeni za shirika la Kivulini.

“Zanzibar tunatekeleza mpango wa kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake, tumekuja kujifunza mbinu hii ya SASA ili nasi ikatusaidie kutekeleza mpango huo” amesema Abdallah

Pia amempongeza Mkurugenzi wa shirika la Kivulini, Yassin Ally kwa jitihada kubwa anazofanya kuelimisha jamii kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally amesema mbinu ya SASA (Start, Awareness, Support & Action) imesaidia jamii kutonyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa wasichana na wanawake ambao sasa wanashiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi pamoja na wenza wao huku matukio ya mimba na ndoa kwa wanafunzi wa kike yakipungua.

“Mbinu hii inashirikisha makundi mbalimbali ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa kuhusu masuala ya ukatili na anachukua jukumu la kuwaelimisha wenzake kukataa ukatili ambapo sisi tumekuwa na jukumu la kuwajengea uwezo,” amesema Ally.

Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdallah wamefanya ziara ya kimafunzo ya siku tatu kuanzia Julai 03,2024 katika shirika la Kivulini ambalo limekuwa likitekeleza miradi ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita na Kigoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here