Dar es Salaam
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa ametoa rai kwa wananchi kupita kwenye banda lao na kupata huduma kwani huduma zote zinazotolewa kwenye ofisi yao zinapatikana hapo.
Akizungumza leo julai 3,2024 kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (DIT) baada ya kupokea tuzo kutoka kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya mshindi wa tatu wa jumla amesema ushindi huo umetokana na utendaji kazi wao.
“Tunapoelekea tunataka kuona kile tulichafanikiwa kukipata leo ndani ya maonesho haya tunataka kiwe kama njia katika utendaji wetu wa kazi,”amesema Nyaisa.
Amesema uwepo wa tuzo hiyo inawakumbusha walipotoka walipo na wanapotakiwa kwenda katika kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha amesema katika maonesho ya mwaka huu hawakuja kuonesha pekee bali wamekuja kufanyakazi kwani watendaji wote wametoka ofisini na kuja kwenye viwanja hivyo kuwahudumia wananchi.
“Nitoe rai kwa wananchi wote kuja kupata huduma hapa hapa kwenye maonesho utasajili kampuni majina ya biashara na vitu vingine na utakabidhiwa cheti chako hapa hapa kwani sasa hatujaja kuonesha tu tunachokifanya bali tumekuja kukifanya kabisa hapa hapa,”amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanafanyakazi kidigitali katika kutoa huduma lakini wafanyakazi wamekuwa na morali ya kufanyakazi ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.