Home KITAIFA WIZARA YA NISHATI YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIASHARA DAR ES SALAAM

WIZARA YA NISHATI YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIASHARA DAR ES SALAAM

📌 Yatoa huduma moja kwa moja kwa Wananchi kupitia Taasisi zake

📌 JNHPP yawa kivutio kikubwa kwa wananchi

Dar es Salaam

WIZARA ya Nishati pamoja na Taasisi zilizo chini yake zinashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 48 yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Katika maonesho hayo Wizara na Taasisi zinatoa elimu ya utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015 pamoja na kutoa huduma za moja mwa moja kwa wananchi.

Pamoja na hayo, Wizara pia inatoa elimu mahsusi kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Katika Banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC)  wananchi wanajionea moja kwa moja shughuli za uchimbaji wa Gesi Asilia, usafirishaji na uchakataji wake kupitia teknolojia ya Uhalisia Pepe ( Virtual Reality) pamoja na kuelezwa juhudi za Serikali katika uendelezaji wa Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

Vilevile,  katika banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wananchi wanaona moja kwa moja utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP) ambao umekuwa kivutio kikubwa kupitia kifaa cha Uhalisia Pepe, pia wananchi wanapata huduma ya kuunganishwa umeme kupitia mfumo katika simu janja wa Nikonekt,  wanapata elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia majiko ya kupikia yanayotunza umeme,  kushughulikiwa changamoto za mita pamoja na kupata elimu ya mabadiliko ya mita za LUKU.

Kupitia Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA)  wananchi wanapata huduma moja kwa moja za Nishati Safi ya Kupikia kupitia wadau wa usambazaji na waendelezaji wa teknolojia husika,  elimu ya usambazaji umeme vijijini na vitongojini na uendelezaji wa miradi midogo ya umeme.

Taasisi nyingine za Wizara ya Nishati zinazoshiriki Maadhimisho husika ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambao wanatoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za udhibiti.

Aidha, kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imejipanga kikamilifu kuonesha miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Ziwa Ngozi na Kiejo-Mbaka.

Maonesho hayo yatafunguliwa na Rais Wa Msumbiji, Filipe Nyusi, tarehe 3 Julai 2024.

Kauli mbiu katika Maonesho hayo ni “Tanzania Mahali Sahihi Pa Biashara na Uwekezaji”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here