Na Leah Choma @Lajiji Digital
WAKALA wa huduma za misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki imetoa rai kwa wananchi kujitokeza kwenye banda lao ili waweze kujifunza vitu mbalimbali na kufaidika na ofa zinazotolewa kwa watakaohitaji kutembela hifadhi za misitu zilizopo nchini.
Akizungumza Julai Mosi 2024 Mkuu wa Kitengo cha Kuhamasisha Utalii wa TFS, Anna Lauwo alipotembelea banda lao lilopo kwenye maonesho ya 48 Kibashara ya Kimataifa Maarufu sabasaba na Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula.
Amesema katika hifadhi za misitu zilizopo nchini zimekuwa na vivutio mbalimbali likiwemo bwawa lenye muonekano wa Ramani ya Afrika na hewa safi.
“Hifadhi zetu zimekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii na ndio maana hapa pia tunatoa kifurushi ambacho tunaweza kumpatia mtu yeyote anaetaka kutembelea hifadhi zetu akija hapa tutamsaidia na kwa bei rahisi sana anaweza kwenda kujionea na kujifunza kwa vitendo,”amesema Lauwo.
Kwa upande wake Afisa Ufugaji Nyuki TFS, Said Abubakar amesema kufuatia umuhimu wa ufugaji nyuki nchini wameanza kutoa elimu kwa watoto ili kuleta hamasa ya ufugaji nyuki lakini pia kuzidi kuifanya nchi kuendelea kuzalisha asali bora Duniani.
Pia Abubakar ametoa wito kwa shule mbalimbali nchini kuanzisha klabu za ufugaji nyuki kama zilivyo klabu nyingine za masomo ili kuendelea kutoa elimu ya ufungaji huo.
Amesema TFS kupitia ofisi zao za kanda wamekuwa wakipokea maombi mbalimbali ya kutoa wa elimu kwa shule lakini pia wanaendelea kutoa elimu kwa mtu mmoja mmoja na vikundi pindi wanapotembelea kwenye ofisi zao.
“Tunapokea watoto wa miaka miwili mitatu ili tuwatengezee hamasa ya ufugaji nyuki kwani wakiwapenda nyuki watafuata nasomo yanayotokana na ufugaji nyuki watatunza mazingira na kupanda maua yakutosha lakini pia wataelewa umuhimu wa mdudu nyuki,”amesema.
“Nipende kutoa rai kwa shule za serikali na shule binafsi kutengeneza klabu za ufugaji nyuki kwani muda muhafaka sasa sisi tupo na tutakua tunawatembea huko na kutoa elimu,” amesema.
Aidha ameongeza kuwa hadi sasa wanashule moja ambayo inaendesha klabu hiyo.
Akizungumzia ujio wa mkutano mkubwa wa kimataifa wa wadau wa ufugaji wa nyuki unaotarajiwa kufanyika Jijini Arusha nchini mwaka 2027 amesema wamejiandaa vizuri hivyo wageni wanatarajiwa kuhudhulia mkutano huo watajionea namna walivyojipanga katika ufugaji na mnyororo mzima wa samani.