Home KITAIFA MKANDARASI ATAKIWA KUHARAKISHA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UMEME WA JUA KISHAPU

MKANDARASI ATAKIWA KUHARAKISHA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UMEME WA JUA KISHAPU

📌Amtaka Meneja kuhakikisha anawasimamia vema mkandarasi

📌Mradi kuleta tija kwenye upatikanaji wa Umeme

Kishapu, Shinyanga

KAMISHNA wa Umeme na Nishati Jadidifu Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga ameridhishwa na hatua mbalimbali za maendeleo katika upatikanaji wa huduma ya Umeme mkoani Shinyanga huku akimsisitiza mkandarasi mradi wa umeme wa Jua wilaya ya Kishapu kukamilisha mradi huo kwa wakati utakaozalisha Megawati 150.

Kamishna Luoga amempongeza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga na menejimenti yake kwa usimamizi mzuri wa miradi ya umeme huku akiwasisitiza wakandarasi kukamilisha kwa wakati miradi inayoendelea ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali.

“Nikupongeze meneja kwa usimamizi mzuri kwa wakandarasi maana ukimsimamia hawezi kuacha kufanya kazi ,mara nyingi sana wakandarasi wanazembea au wanakimbia ni kwa sababu tu haupo usimamizi mzuri kwahiyo ongezeni usimamizi kwa hao wakandarasi ikiwa ni pamoja na kutembelea miradi na kufanya nao vikao vya mara kwa mara ili kujua changamoto na maendeleo ya miradi,” amesisitiza Mhandisi Luoga.

Kuhusu masuala ya usimamizi kwenye miundombinu na uharibifu unaofanyika Mhandisi Luoga amesema ,wale wanaofanya kwa makusudi au kwa kutokujua wanapaswa kupatiwa elimu kuhusu athari za uharibifu wa miundo mbinu hiyo na namna ya kuilinda.

Amesisitiza kuwa mradi huo wa umeme wa Jua ni muhimu sana kwani mara baada ya kukamilika utaongeza kiasi cha uzalishaji umeme nchini pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Pia, amewataka wakandarasi kuhakikisha hawacheleweshi utekelezaji wa mradi wa Jua wa Kishapu na waukamilishe kwa ubora wa hali ya juu na kuongeza kuwa kipaumbele cha ajira kitolewe kwa wanawake.

Awali, akisoma taarifa ya miradi ya kusambaza umeme kwa mwaka wa fedha 2023/2024 meneja wa shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Leo Mwakatobe amesema, mradi wa umeme wa jua unaotekelezwa katika maeneo ya Ngunga Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga umefikia asilimia kumi (10) ambapo unatarajiwa kukamilika Mwezi Februari 2025.

“Hali ya usambazaji Umeme imeendelea kuimarika kutokana na miradi mbalimbali ya kusambaza Umeme inayotekelezwa na TANESCO na ile ya kusambaza Umeme vijijini inayofadhiliwa na serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA),”amesema.

Kamishna Luoga amekagua pia mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ibadakuli pamoja na mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Ibadakuli hadi Simiyu.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Leo Mwakatobe pamoja na mambo mengine amesema shirika hilo linasimamia miradi miwili ya kimkakati ambayo ni mradi wa Umeme wa Jua Wilaya ya Kishapu pamoja na mradi wa kuboresha upatikanaji Umeme Bulyanhulu ikiwa lengo ni kuongeza uzalisha Umeme na kuboresha upatikanaji Umeme.

“Mradi wa Umeme wa Jua, kutokana na mahitaji ya Umeme kuongezeka serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Umeme Jua maeneo ya Ngunga Kishapu ili kuongeza kiwango cha upatikanaji Umeme Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine ya Nchi, mradi huu unatarajiwa kuzalisha Umeme wa kiasi cha Megawati 150 ambapo mradi unathamani ya ya zaidi ya bilioni 300 na umegawanyika katika awamu mbili ya kwanza ni MW 50 na mkandarasi ni SINOHYDRO ambapo mkandarasi ameshakabidhiwa kazi na kuanza ujenzi Mwezi Oktoba 2023, na kwa sasa mradi upo asilimia 10 na matarajio ya kukamilika ni baada ya Miezi 14,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here