Home AFYA MAABARA YA MUHIMBILI MLOGANZILA YAPAA KWA UBORA KIMATAIFA

MAABARA YA MUHIMBILI MLOGANZILA YAPAA KWA UBORA KIMATAIFA

Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa mara nyingine imepata cheti cha Ithibati ya Ubora Kimataifa kutoka Shirika la Viwango vya Ukaguzi Kimataifa (SADCAS) kwa mwaka 2023/2024 baada ya SADCAS kujiridhirisha juu ya mwenendo wa utoaji wa huduma bora kwa jamii kutoka maabara hiyo.

Hayo yamesemwa leo Juni 28 na Mkurugenzi Mtendaji MNH, Profesa Mohamed Janabi wakati akipokea cheti hicho na kuongeza kuwa cheti hicho cha ithibati kimeongeza wigo wa vipimo kutoka vipimo 17 2021/2022 hadi kufikia vipimo 44 mwaka 2023/2024

“Kupitia cheti hiki cha ubora vipimo vinavyofanyika hapa Mloganzila majibu yake yanafanana na majibu kutoka maabara yoyote duniani, kwahiyo hii inadhihirisha namna ambavyo wataalam wetu wanafanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Shirika la Afya Duniani pamoja na ile ya Wizara ya Afya,” ameongeza Profesa Janabi.

Ameongeza kuwa kufuatia ithibati hiyo Maabara ya Mloganzila itakuwa kituo cha mafunzo na utafiti, inaweza kupokea na kupima sampuli kutoka sehemu mbalimbali na kutoa majibu sahihi kwa wakati, kuaminika kwa ubora wa vipimo na majibu kimataifa.

Amesema hivyo sampuli ya vimelea vitakavyopimwa katika maabara hiyo vinaweza kutumiwa na mamlaka au taasisi yoyote duniani.

Aidha, Profesa Janabi amewataka wataalam hao wa maabara kuendelea kuchapa kazi kwa weledi ili kulinda ubora uliopo na kuifanya maabara hiyo kuendelea kuaminika nje na ndani ya Tanzania.

Kwa upande wake Afisa Ubora wa Maabara MNH-Mloganzila Lanja Kahemela amesema ukaguzi uliofanywa na SADCAS umezingatia mwongozo mpya wa ubora kutoka ule wa zamani (ISO15189:2012 kwenda ISO15189:2022) ambapo unasisitiza kumfikia mgonjwa ikiwemo kuangalia usalama wake zaidi.

Itakumbukwa kuwa Maabara ya Muhimbili Mloganzila ni miongoni mwa maabara kubwa nchini ambayo inapima zaidi ya vipimo 1000 kulingana na idadi ya wateja wanaofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here