Home KITAIFA SERIKALI ZOTE MBILI BARA NA VISIWANI ZINA VIONGOZI WENGI WANAWAKE: WAZIRI RIZIKI

SERIKALI ZOTE MBILI BARA NA VISIWANI ZINA VIONGOZI WENGI WANAWAKE: WAZIRI RIZIKI

Esther Mnyika, Dar es Salaam

WAZIRI wa maendeleo ya Jamii kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Riziki Pembe Juma amesema Serikali zote mbili bara na visiwani kwa sasa zina viongozi wengi wanawake kutokana na marais wa pande zote mbili kutokuwa na ubaguzi wa kijinsia hivyo kuwachagua wanawake wenye uwezo wa kuongoza.

Hayo ameyabainisha Juni, 24 wakati wa Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake katika Diplomasia yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuwaunganisha pamoja wanawake katika masuala mazima ya kidiplomasia na Tanzania miongoni mwa nchi zenye viongozi wengi wanawake akiwemo mwanadiplomasia namba moja Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

“Serikali zote mbili zimetambua uwepo wa wanawake kwa kuwachagua katika sekta mbalimbali ikiwemo mawaziri ambapo sasa kwa Zanzibar wanawake waliopo katika nafasi za maamuzi ni asilimia 33,” amesema Pembe.

Ameeleza kuwa uwepo wa maadhimisho hayo hapa nchini ni jitihada ya serikali zote za Muungano katika kuhakikisha inamuwezesha mwanamke kuingia katika nyanja zote maamuzi.

Akizungumzia kuhusu uchumi Pembe amesema serikali zote zimeweka miundombinu ya kuwainua wanawake ikiwemo kuwapa kipaumbele katika kuwapa mikopo isiyokuwa na riba.

“Wanawake wamepewa kipaumbele kila sehemu kwenye siasa tunae Jemedari wetu Rais Dkt Samia,ukienda kwenye uchumi wanawake wapo,kwenye elimu,Afya kote serikali imeweka mazingira mazuri kuhakikisha mwanamke anapata nafasi,”ameongeza.

Amesema Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wanawake katika Diplomasia “Ni kuadhimisha mafanikio na michango ya wanawake katika Diplomasia na ushirikiano wa kimataifa”.

Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wake anaoufanya kwa kuzingatia jinsia kwani umepelekea nchi kuwa na wanawake asilimia 24 katika Diplomasia.

Amesema kwa mara ya kwanza yanaadhimishwa nchini tangu kuhasisiwa kwake mwaka 2022 na Baraza la Umoja la Mataifa.

Amesema Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika ngazi ya maamuzi kwa kuhakikisha anawachangua katika nafasi mbalimbali za maamuzi.

“Katika kutambua mchango wa wanawake katika diplomasia leo hapa tupo na wanadiplomasia nguli kutoka ndani ya nchi na nje tunae Balozi Getrude Mongera,Balozi Amina Salum Alli,barozi Riberata Mulamula na maborozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa”,mesema Balozi Mussa.

Siku ya wanawake katika diplomasia huadhimishwa Juni 24 kila mwaka na ilianzishwa ili kutambua na kuthamini juhudi za wanawake ambao wamejitolea maisha yao katika nyanja za diplomasia na uongozi wa kimataifa wanawake wamekuwa na msaada mkubwa katika kujenga madaraja kati ya mataifa, kukuza ushirikiano wa kimataifa na kutafuta suluhisho la migogoro kwa njia ya amani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here