Home MICHEZO MICHUANO YA SHIMIWI KUFANYIKA SEPTEMBA 2024

MICHUANO YA SHIMIWI KUFANYIKA SEPTEMBA 2024

Dodoma

MAANDALIZI ya michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yameanza ambapo Kamati ya Utendaji imependekeza michuano hiyo kufanyika Septemba 2024 mkoani Morogoro.

Timu zinazoshiriki michezo hiyo zimehimizwa kufanya maandaalizi kwa watumishi wa serikali kutoka kwenye wizara, taasisi, wakala za serikali, ofisi za wakuu wa mikoa na halmashauri na manispaa ili kushiriki bonanza la uzinduzi litakalofanyika Agosti jijini Dodoma na hatimaye michuano ya SHIMIWI mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Alex Temba amesema mgeni rasmi wa bonanza hilo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka ambaye ni mlezi wa Shirikisho hilo.

Temba amesema michezo itakayofanyika kwenye bonanza hilo litakalofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ni pamoja na kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, mpira wa miguu, netiboli na mbio za watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 55

“Tarehe rasmi ya michezo yetu pamoja na hili bonanza kubwa itatangazwa baadaye mwezi huu maana ni utaratibu wetu lazima michezo itanguliwe na bonanza kubwa lenye kushirikisha watumishi wa umma wenye kushiriki kwenye michezo hii ya SHIMIWI,” amesema Temba.

Aidha amezitaka timu kuanza kuandaa timu zao kwa ajili ya kushiriki kwenye bonanza hilo, ambapo amesema rekodi inaonesha ushiriki wa klabu kwenye michezo hii unaendelea kuongezeka kutoka 47 kwa mwaka 2021 na kufikia 62 ilikuwa mwaka 2022, na 2023 kulikuwa na klabu 74.

Kikao hicho kimeudhuriwa pia na Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba ambaye awali alitoa wito kwa timu kuanza maandalizi ya michezo ya SHIMIWI, ili kuleta ushindani bora kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Mwalusamba amesema kwa kuwa mwaka huu michezo itatanguliwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa, ametoa wito kwa watumishi kuelekeza akili zao pia katika maelekezo ya watendaji wakuu wa serikali kuhusiana na uchaguzi huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here