Dar es Salaam
BANDARI ya Dar es Salaam imeweka rekodi kwa kupokea meli kubwa ya mizigo yenye urefu wa mita 294.1 tofauti na meli ambazo imewahi kuzipokea hapo awali kwani meli ya mwisho kupokelewa ilikuwa na urefu wa mita 267 hatua inayotafsiriwa kama sehemu ya mafanikio ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwa meli hiyo kwenye Bandari ya Dar es Salaam jana, Meneja Mizigo Mchanganyiko wa Banadari ya Dar es Salaam, Abed Gallus amesema kuwa meli ya (MSC ADU -V) imekuwa meli ya kwanza kubwa kuwasili katika bandari hiyo kwani ina uwezo wa kubeba makontena 4000.
“Hii ni historia kwetu kwani hapo awali tulikuwa tunapokea meli zenye urefu wa mita 267 lakini sasa tunauwezo wa kupokea meli zenye uwezo ukubwa wa mita 305 haya ni mafanikio makubwa kwetu kama Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA),” amesema Abed.
Amesema uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia TPA katika Bandari ya Dar es Salaam umechangia kiasi kikubwa kuongezeka ufanisi wa kiutendaji ambapo awali likuwa na kina cha wastani wa mita 8 mpaka 12.7 lakini sasa kimeongezwa na kufikia mita 14.5 na kuwa na uwezo wa kupokea meli yenye urefu wa mita zaidi ya 305.
“Tunazipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya ambayo imewekeza vya kutosha katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kuongeza kina na vitendea kazi katika bandari yetu na hivyo kutoa matokeo chanya ikiwemo kuanza kupokea meli kubwa,” amesema.
Aidha , Abed amesema moja ya faida ya kubwa kupokea meli kubwa za mizigo ni kupungua kwa gharama za kusafirisha mizigo ambapo italeta unafuu kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo sambamba na kuchochea ushindani wa bandari zilizopo ukanda wa Afrika mashariki na kati.
“Kumekuwa na ufanisi mkubwa ikiwemo kuhakikisha upakuaji wa mizigo unafanyika kwa haraka zaidi kwani ndani ya masaa 24 tuna uwezo wa kupakua wastani wa makontena 800 hivyo tunatarajia ndani ya siku tano meli hii itakuwa imeshapakia na kuondoka katika bandari yetu,” amesema.
Abed amesema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwa bandari sita ambazo TPA inazisimamia na kwa kuliona hilo Mamlaka imeendelea kuboresha bandari nyingine ili kutoa msaada kwa Bandari ya Dar es Salaam ambayo zaidi ya asilimia 95 ya mizigo inapita katika bandari hiyo.
“Tumendelea kuboresha miundombinu ya bandari zetu ikiwemo pamoja na bandari ya Mtwara na Tanga ambapo tayari tumeshanunua vifaa vya upakuaji mizigo kwani hapo awali Bandari ya Tanga, meli zilikuwa zinafungwa nje ya gati lakini sasa hivi meli zinaingia kwenye gati. Maboresho haya yote ni juhudi za mamlaka kuhakikisha bandari hizo zinatoa msaada kwa Bandari ya Dar es salaam,” amesema Abed.
Katika kufanya kazi kiushindani sambamba na kujiimarisha kibiashara, TPA imeingia mikataba ya kiuendeshaji katika baadhi ya gati zake kwa Bandari ya Dar es salaam, kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi na hivyo kufanya bandari hiyo kuwa kinara kwa uingizaji na usafirishaji wa mizigo kwa nchi nyingi zikiwemo za maziwa makubwa na kusini mwa jangwa la Sahara.