Home MICHEZO MUHIMBILI YAJIDHATITI KWA UCHUNGUZI NA MATIBABU AFCON

MUHIMBILI YAJIDHATITI KWA UCHUNGUZI NA MATIBABU AFCON

Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) imejiandaa kikamilifu katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wachezaji watakaoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 yanayoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF).

Kauli hiyo imetolewa Juni, 18 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Mohamed Janabi wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu namna hospitali hiyo inavyoendelea kuboresha huduma za ubingwa bobezi hapa nchini na kuwa kimbilio kwa watanzania wengi.

“Hospitali ya Taifa Muhimbili ndio hospitali kubwa kuliko zote Afrika Mashariki, tuna vitanda 2300 kwa kampasi zote mbili, tuna wataalam bingwa bobezi wengi ukilinganisha na hospitali zingine, pia tuna huduma za ubingwa bobezi ambazo baadhi yake hazipatikani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki hivyo hakuna sababu kwa wachezaji hao kutoletwa kwetu kwa matibabu,” amebainisha Profesa Janabi

Ameongeza kuwa utoaji huu wa huduma bora unatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kusomesha wataalam, ununuzi wa vifaa tiba, dawa na vitendanishi.

Aidha, Profesa Janabi amevishauri vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya NBC kuleta wachezaji wao kwa ajili ya kufanyiwa vipimo kabla ya wachezaji kupewa mikataba ya kuzitumikia klabu hizo kwakuwa baadhi yao wanaweza kuwa na changamoto za kiafya zinazoweza kusababisha wasitumikie klabu hizo kwa ufanisi.

Itakumbukwa kuwa Tanzania imechaguliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kushirikiana na Kenya pamoja na Uganda mwaka 2007.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here