Na Esther Mnyika@Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji (Rufaa) Jacob Mwambegele amesema Tume inaheshimu na kutambua mchango wa vyombo vya habari vya kijamii na kidigitali haswa katika kuwafikia vijana ambao ndio walengwa wakubwa wa zoezi la uboreshaji wa daftari.
Pia amesema Tume imeanza mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, na uboreshaji huo utazinduliwa mkoani Kigoma Julai 1 Mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa Majaliwa .
Akizungumza leo Juni,13 2024 kwenye mkutano wa Tume na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani city jijini Dar es Salaam wenye lengo la kutoa taarifa mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kuanza rasmi zoezi la uboreshaji wa daftari.
Amesema Tume inaamini kuwa uwepo wa uwakilishi huo mpana wa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwenye mkutano huo utasaidia katika kuongeza wigo wa wakuwafikia wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla haswa katika kipindi hiki cha uboreshaji wa daftari la kidumu la wapiga kura.
“Tunawasihi muendelee kutuunganisha na wadau,Tume kwa upande wake itaendelea kuweka milango wazi kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara,“amesema.
Amesema tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba vyombo vya habari vikuu bado vinawafikia watu wengi na vina umuhimu mkubwa katika kuwahabarisha na kuelimisha wananchi.
Amesema Tume katika kipindi chote cha uboreshaji wa daftari itakuwa na kituo cha huduma kwa wateja ,kupitia kituo hicho wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla wanaweza kupiga simu na kujibiwa maswali mbalimbali yanayohusiana na uboreshaji wa daftari.
Akizungumzia kuhusu maandalizi hayo pamoja na mambo mengine yanajumuisha uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura,uboreshaji wa majaribio,ununuzi wa vifaa na ushirikishwaji wa wadau .
Amesema jukumu hilo pia limeanishwa kwenye kifungu cha 16 (5) cha sheria ya uchaguzi wa Rais ,wabunge,na madiwani namba 1 ya mwaka 2024 ambacho kinaweka sharti kwa Tume kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi Mkuu uliomalizika na Kabla ya siku ya uteuzi wa wagonbea kwa ajili ya uchaguzi Mkuu unaofuata .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Kailima, Ramadhani akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza alisema kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tatehe ya uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Ameongeza kuwa itatoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine.
Akizungumzia idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa kupiga kura amesema wapiga kura wapya wanaotarajiwa ni 5,586,433 kati ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20.
Amesema wapiga kura 4,369,531 wanatarajia kuboresha taarifa zao wakati wapiga kura 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendeleo kuwepo kwenye daftari hilo ambapo baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa Daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura 34,746,638.
“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikua na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/20 lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura”,amesema Kailima.
Amesema Tume tayari imekamilisha maandalizi yote ikiwemo vituo vya kuandikishia wapiga kura ambapo vipo vituo 40,126 nchi zima Tanzania bara na Zanzibar.