Home AFYA DK. MBONEA: JAMII IJITOKEZE KUCHANGIA DAMU KUKIDHI MAHITAJI MKUBWA

DK. MBONEA: JAMII IJITOKEZE KUCHANGIA DAMU KUKIDHI MAHITAJI MKUBWA

Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imetoa wito kwa jamii nchini kujitokeza kuchangia damu ili kukabiliana na uhitaji wa damu uliopo hospitali hapo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi MNH, Dk.Yonaz Mbonea wakati akifungua hafla fupi ya kutambua mchango wa wachangiaji damu ambayo huadhimishwa Juni 14 kila mwaka na kuongeza kuwa hospitali ina uhitaji mkubwa wa damu takribani chupa za damu 120 kwa siku kutokanana idadi kubwa ya wagonjwa wanaopokelewa hospitalini hapo.

Dk. Mbonea ameongezea kuwa, hospitali imekua ikishirikiana na mpango wa taifa wa damu salama, shule, taasisi za kidini na wachangiaji damu binafsi ili kusaidia upatikanaji wa damu.

“Takwimu zinazonyesha kuwa kipindi cha Januari mpaka Machi mwaka huu makusanyo yetu ya damu yameongezeka kufikia chupa 5,847 ni sawa na ongezeko la asilimia 65” ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo tulikusanya chupa za 3,540,”amesisitiza Dk. Mbonea.

Kwa upande wake, Godian Gabriel ambaye ni mchangia damu amesema ameanza kuchangia damu mwaka 1998 na ametoa damu mara 55 na kuhimiza kuwa na upendo kwa jamii yetu iliyotuzunguka ili kuweza kuwa wachangia damu wazuri maana uhitaji ni mkubwa.

Kauli mbiu ya Siku ya kuchangia damu Duniani ni “Changia damu, Changia sasa, Changia mara kwa mara”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here