Dar es Salaam
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan mesema yoyote anayetaka kumkera amkanyagie uchumi ambao sasa umekuwa katika mageuzi makubwa.
Pia amesema mageuzi ya kiuchumi anayoifanya nchini inasababisha anatukanwa na kupigiwa kelele nyingi lakini amejigeuza chura kiziwi ambaye atosikiliza mambo hayo bali ataendelea kutimiza malengo na mipango yake.
Rais Dk.Samia hayo ameyasema leo Juni ,11 2024 Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kukabidhi gawio kwa serikali kutoka kwenye mashirika ya umma na binafsi, hafla hiyo yenye kauli mbiu ‘Mageuzi ya mashirika ya umma na wajibu wa kuchangia maendeleo ya Tanzania’.
Amesema anayasikia matusi anayotukanwa lakini amejigeuza chura kiziwi ambaye hayasikii wala kujibu bali anachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi ili maendeleo yapatikane.
“Kulikuwa na mashindano ya chura, waliwekewa tageti atakayefika juu atapatiwa zawadi, walipoanza kupanda huku chini watazamaji wakaanza kuwaambia shukeni ni hatari hamtaweza kufika mtashindwa tu, kelele zilikuwa nyingi kama zinazopingwa humu ndani kwetu, kwahiyo chura mmoja mmoja akaanza kushuka ila akabaki mmoja akaulizwa umewezaje kufika kumbe yule chura kiziwi asikii.
“Mimi kazi mliyonipa nasimama na naifanya na mnashuhudia matusi ninayotukanwa, mpuuzi huyo hana maana huyu bibi mambo chungu nzima lakini najigeuza chura kelele zinapigwa nyingi wakiona haujibu wanasema sasa tulitukane litajibu mimi sijibu masikio sisikii kabisa anayetaka kunikera anikanyagie uchumi wangu,” amesema Dk. Samia.
Amesema matusi yanayoendelea katika mitandao ya kijamii anayaona ila anakaa kimyaa kwani lengo lake ni kufanya mageuzi ya kiuchumi na siyo vinginevyo.
Amesema kwenye mageuzi haya Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu na Waziri wake wanatakiwa kuendelea kufanyakazi kwakuwa anajua kuwa watachukiwa na kulaaniwa na baadhi ya watu wasiopenda kufanya kazi.
“Kwenye mageuzi haya Mchechu na Waziri wako lazima muwe ‘unpopular, sijawahi kusikia Waziri wa fedha akasifiwa hata siku moja siku zote analaaniwa, kwahiyo Mchechu najua hapa utalaumiwa, lawama zingine zitakuja personal nyingine kikazi lakini hii ndiyo kazi niliyokupa,” amesema.
“Kwenye mageuzi haya tutakanyaga nguru wa mshihiri, kwahiyo anayetaka kunikera mimi anikanyagie uchumi wangu, najua katika mageuzi haya tutawakanyanga wengi hasa wale ambao hawataki kwenda mbele na ndio watapiga kelele nyingi sana, mliopo kwenye shirika ambao hamtaki kukanyagiwa nguru wenu nendeni mkafanye kazi ili kuleta maendeleo,” amesema.
Kuhusu kuuzwa kwa bandari Dk. Samia amesema kuwa anaipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kutoa gawio kwa serikali kiasi cha Bilioni 153.9 na kwamba wanaopiga kelele kuwa ‘mama kauza bandari’ ni wazi kuwa wameona faida ya uwekezaji uliyofanyiwa bandarini hayo.
Amesema anaamini kuwa TPA itaendelea kupata faida na kutoa gawio kubwa zaidi kwa serikali hasa kutokana na mageuzi hayo yaliyofanyika.
Aidha ametoa Pongezi maalum kwa makampuni yaliyoleta gawio kwa serikali ikiwemo TPA ambayo nina uhakika mwaka jana hiyo haikuwa level yenu, lakini kwa mageuzi yaliyotokea bandarini wameweza kufikia kiwango hicho na mwakani ana uhakika wanaweza kuleta double ya walichokitoa leo.
“Huko ndiko tulikuwa tunaelekea ndugu zangu, wale waliokuwa wanapiga kelele mama kauza bandari, mama kauza bandari, mama kauza nini, mauzo yale faida yake ni hii hapa na huu ni mwanzo tu tunatarajia kupata faida kubwa zaidi,” amesema Dk. Samia
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema ili kuyafanya. Mashirika ya Umma yawe na umiliki wa wananchi, Serikali inakamilisha mchakato wa kuyaandikisha kwenye soko la hisa ili wananchi wanunue hisa na wayamiliki.
Ameeleza kuwa kuhusiana na utekelezaji wa zoezi la kufuta au kuunganisha mashirika yasiyofanya vizuri ama kupitiwa na wakati wapo katika hatua za mwisho kukamilisha zoezi hilo na hivi karibuni watatoa taarifa.
“Katika mageuzi haya inaonekana ni vema kuyaandikisha mashirika yote kwenye soko la hisa na wawe na umiliki wa moja kwa moja wa mashirika haya,”amesema Profesa Mkumbo.
Amefafanua kuhusu mashirika yakayounganishwa wanyeviti wa bodi na watendaji wakuu wawe tayari mmoja kubaki katika nafasi hiyo au wote kuondolewa kama ambavyo itampendeza mwenya mamlaka.
Amesema umuhimu wa taasisi zao ni kuhakikisha zinachangia uchumi na kupunguza mzigo kwa serikali.
Akizungumza Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu wkati akitoa taarifa ya kupokea gawio na michango kutoka kwa Mashirika na Taasisi amesema ni wajibu wao watendaji wote kuchangia gawio kwa serikali kwa ujumla kutoka kwenye taasisi hizo.
Amesema hadi sasa wametoa gawio shilingi bilioni 637 bado hawajafikia lengo wanatarajia shilingi bilioni 850 kufikia mwisho wa mwaka huu.
Aidha amewataka watendaji wakuuu na Wakurugenzi wa mashirika ya umma wawe tayari kwa mabadiliko yatakayowawezesha kubadili namna yao ya kuendesha mambo na kutoa gawio kwa serikali.
Pia amesema watendaji hao kuhakikisha wanaongeza ubinifu na kukuza mapato ya taasisi zao ili yaweze kuingia kwenye mfuko mkuu wa serikali na kusaidia katika maendeleo ya Taifa
“Gawio linatolewa na taasisi za umma ni chini ya asilimia tatu na hivyo lazima mabadiliko makubwa yafanyike kufikia lengo la serikali la kupata gawio kwa asilimia 100,” amesema Mchechu.
Amesema taasisi ambazo serikali ina asilimia ndogo inachangia fedha nyingi katika mfuko mkuu wa serikali tofauti na mchango mdogo unatolewa na taasisi zinazomilikiwa na serikali kwa asilimia 100.
Ameongeza kuwa ofisi yake imekusidia kuja na mfumo thabiti ili kusaidia serikali kufanya uamuzi sahihi wakati wa uteuzi wa viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali.
Mchechu amesema mifumo hiyo itaondoa changamoto ya kuteua na kutengua ndani ya muda mfupi baada ya kuteuliwa.
“Wakati mwingine tunaona aibu kujieleza pale ambako hatukufanya vizuri lakini nitoe mfano hair kwa nini tunapaswa kutengeneza mfumo mzuri wa kuangalia taarifa za utendaji kazi wa wakuu wa taasisi, siku moja wakati unaapisha hapa kuna wenzetu mmoja aliondolewa baada ya siku moja,”amesema.
“Tunaomba tukuhakikishie Rais Dk. Samia kuwa tutakwenda kufanya mabadiliko na mabadiliko lazima yawepo watu wengi huwa hatupendi mabadiliko lakini matunda ya mabadiliko siku zote huwa ni neema sana,”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongo(NCAA), Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo amesema bodi za mashirika ya umma na taasisi zingine zina wajibu wa kulinda maslahi ya umma kwa kusimamia utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji mapato
Amesema kuundwa kwa taasisi hizo ilikuwa ni kuwezesha serikali kukusanya mapato kwaajili ya kuwahudumia wananchi lakini kuongeza uwekezaji na kutoa ajira na kufungua fursa zaidi za uchumi.