Home AFYA MUHIMBILI MLOGANZILA SULUHISHO LA MATIBABU YA NYONGA NA MAGOTI

MUHIMBILI MLOGANZILA SULUHISHO LA MATIBABU YA NYONGA NA MAGOTI

Dar es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi amesema MNH-Mloganzila imeendelea kuimarisha na kuanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa nyonga na magoti bandia kwa lengo kusogeza huduma karibu na wananchi kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Profesa Janabi amesema hayo Juni 10 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati wa tukio la kumruhusu mchezaji wa zamani wa Klabu ya Yanga na Timu ya Taifa, Mzee Sunday Manara baada ya kufanyiwa upasuaji wa kupandikizwa goti bandia ambapo sasa anaendelea vizuri.

Ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja MNH-Mloganzila imefanya upandikizaji wa nyonga na magoti bandia kwa wagonjwa takribani 163 ambapo kati yao waliopandikizwa magoti bandia ni 112 na nyonga bandia ni 41, na wote wanaendelea vizuri.

“Pamoja na familia ya mzee Sunday Manara kuwa na uwezo wa kumpeleka mzee wao nje ya nchi kwa matibabu walituamini na kuamua kumleta hapa MNH Mloganzila, tumemfanyia tarehe sita mwezi huu, leo tutamruhusu kurudi nyumbani kwa kuwa afya yake imeimarika sana na baada ya miezi mitatu atarejea kwenye shughuli zake kama kawaida,” amebainisha Profesa Janabi.

Kwa upande wake Mzee Sunday Manara ameipongeza serikali kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya na kuwafanya wataalam wa ndani kutoa huduma za ubingwa bobezi ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi kwa gharama kubwa kulinganisha na kipato cha Watanzania walio wengi.

Mzee Manara ameishauri jamii kuto kaa na maumivu kwani Muhimbili Mloganzila wanatoa huduma nyingi za ubingwa bobezi kwa teknolojia za kisasa, huduma zao ni nzuri kuanzia mapokezi, lugha na pia ufuatiliaji wa mgonjwa pindi anapokuwa wodini.

Kwa upande wake Daktari Bingwa Bobezi wa Mifupa, Nyonga na Magoti, Dk. Abubakar Hamis amesema tatizo la magoti linaweza kusababishwa na uzito mkubwa na ajali ambapo maumivu huanza kidogo kidogo na baadaye yanaweza kusababisha mgonjwa kushindwa kutembea na hatimaye ulemavu, lakini akipandikizwa magoti bandia maumivu yanaisha kabisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here