Home KITAIFA DK. NCHEMBA: UJENZI WA KITUO CHA FORODHA HUZINGATIA UCHUMI NA USALAMA

DK. NCHEMBA: UJENZI WA KITUO CHA FORODHA HUZINGATIA UCHUMI NA USALAMA

Na. Peter Haule, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amemshauri Mbunge wa Ngara, Ndaisaba George Ruhoro kushirikiana na Mamlaka husika ili kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma, mkoani Kagera baada ya kujiridhisha pasipo shaka iwapo eneo hilo linafaa kwa ujenzi wa Kituo hicho.

Dk. Nchemba amesema hayo bungeni, jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Mhe. Ndaisaba George Ruhoro, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma.

Amrsema endapo Mamlaka husika zitajiridhisha pasipo shaka kuhusu eneo hilo kutokuwa na madhara kwa nchi kiuchumi, kijamii na kiusalama, Serikali itashauriwa kuyafanyia kazi maombi hayo.

“Kabla ya eneo au kituo kuteuliwa kuwa eneo la Forodha na kuweza kufunguliwa kama kituo cha forodha mahali popote nchini kuna taratibu za kisheria ambazo inabidi zifuatwe,”amesema Dk. Nchemba.

Ameeleza utaratibu huo kuwa ni pamoja na kutangazwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya Mwaka 2004, Kifungu Namba 11.

Dk. Nchemba amesema baada ya Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa kupokea maombi ya kuteua eneo husika kuwa eneo la forodha kutoka kwa Waziri mwenye dhamana, huwasilisha pendekezo la kuteua kituo husika kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here