Na. Peter Haule, Dodoma
SERIKALI imesema kuwa hadi Machi 2024 imelipa jumla ya shilingi bilioni 949.31 sawa na asilimia 92 ya madeni ya wazabuni wa bidhaa na huduma pamoja na wakandarasi yaliyohakikiwa kati ya madai yaliyowasilishwa yenye thamani ya shilingi trilioni 1.03.
Hayo yamesemwa leo Juni 10 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Geoffrey Mwambe, aliyetaka kufahamu hadi sasa Serikali inadaiwa kiasi gani na wazabuni, wafanyabishara, wakandarasi na walipa kodi kutokana na huduma, kazi na kodi zilizozidi.
Dk. Nchemba amesema kuwa kati ya kiasi cha shilingi trilioni 1.03 cha madeni yaliyohakikiwa hadi machi 2024 shilingi trilioni 1.02 ni madeni ya wazabuni wa bidhaa na huduma na shilingi bilioni 8.75 ni madeni ya wakandarasi.
Amesema kuwa hadi kufikia Machi 2024, Serikali ilikuwa inadaiwa jumla ya shilingi bilioni 80.06 ya madeni yaliyohakikiwa yanayotokana na kodi (VAT Refunds Claims) na imefanya marejesho ya jumla ya shilingi bilioni 675.1 sawa na asilimia 96 ya lengo kwa kipindi hicho.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Adamson Mwakasaka, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwalipa wastaafu kwa wakati mafao yao, Dk. Nchemba, amesema kuwa Serikali imeishasimika Mfumo wa Malipo ya Pensheni – TPPS kwa wastaafu wanaolipwa mafao na Hazina pamoja na kuskani majalada yote ya wastaafu na kuyahifadhi katika Mfumo wa Malipo ya Pensheni.
Amesema kuwa hatua hiyo imesaidia mstaafu kupata taarifa na majibu yake kwa haraka wakati wanapotembelea Ofisi za Hazina Ndogo zilizopo mikoa yote nchini.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na mafao ya hitimisho ili Mstaafu ajue mfuko sahihi anaopaswa kulipiwa na aina ya mafao atakayostahili kulipwa.