Zanzibar
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania Suzan Peter Kunambi amewataka Wanawake,Wanachama na Viongozi wa Jumuiya hiyo kuwa na Umoja,Mshikamo na Nguvu ili kuendelea kuwa na Jumuiya imara inayotegemewa na Chama Cha Mapinduzi.
Katibu Mkuu Kunambi amesema Chachu na kasi iliyopo sasa chini ya Viongozi wa UWT Taifa ilete hamasa na ari kwa wanawake wote nchini sambamba na viongozi wa ngazi zote kuwajibika ipasavyo.
Katibu Mkuu Kunambi amesema hayo leo Juni 9, 2024 alipokuwa akihutubia mamia ya Wanawake na wana CCM waliokuwa kwenye viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar wakati wa Shamra Shamra za kumpokea tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa UWT na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Mei 19, 2024.
“Jumuiya ya UWT ni imara na chama inaitegemea,hivyo tunapaswa kuwa na umoja na mshikamano ili kuwa na nguvu na kuwaunga mkono viongozi wetu wa juu Mwenyekiti wetu wa CCM na Rais Dk. Samia pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dk. Mwinyi,”amesema Kunambi.
“Viongozi wetu wa Jumuiya ya UWT Taifa Mwenyekiti Mary Chatanda na Makamu Mwenyekiti Zainab Shomari ni wachapakazi walioleta mabadiliko makubwa ndani ya UWT,”amesema.
Katibu Mkuu Kunambi pia amesisitiza kuwa UWT imejidhatiti kuhakikisha Wanawake wanashiriki kwenye kugombea nafasi za uongozi kwenye Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu 2024 na uchaguzi mkuu mwakani 2025.