Na Chedaiwe Msuya, Kigoma
WANANCHI wametakiwa kukopa mikopo yenye faida kwenye taasisi au mtu binafsi ambaye ana leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania ili kuwa na uhakika wa mkopo na kuondoa changamoto kwa wananchi hao.
Wito huo umetolewa katika Kata ya Mabamba, Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma na Afisa Usimamizi wa Fedha katika Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma.
“Hakikisha unapokwenda kukopa, mkopeshaji awe na leseni kwa kuwa mtoa huduma huyo atakuwa amekidhi vigezo na masharti vilivyowekwa na mamlaka husika”, amesema Kibakaya.
Aidha, amewahimiza wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kuweka akiba ili kuweza kutambua mapato wanayo yapata kupitia biashara zao
Amesema wakitunza fedha lazima wawe na malengo ili akiba hiyo iwe na faida na pia ni vema wahifadhi fedha kwenye akaunti za Benki au kwenye simu, sehemu ambazo ni salama ili kuepuka hasara au upotevu.
Kuhusu uwekezaji, Kibakaya, amesema kuwa jambo hilo si kwa ajili ya watu wenye kampuni kubwa pekee bali hata mwananchi wa kawaida anaweza kuwekeza kupitia biashara ndogondogo anazozifanya.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mabamba, Wilayani Kibondo, Shedrack Chongela, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa elimu waliyoitoa kwa wananchi hao huku akiwakumbusha wananchi wanapokwenda kuchukuwa mikopo waende maeneo yenye kukidhi vigezo.
Naye Mkazi wa Kijiji cha Mabamba, Wilaya ya Kibondo, Felister Kazombe, amesema kuwa semina hiyo ni muhimu kwa jamii yao kwa kuwa imetoa mwongozo mzuri kuhusu masuala ya fedha.