Home KIMATAIFA TAASISI YA MSAADA WA KISHERIA AFRIKA (ALSF) KUWAJENGEA UWEZO WANASHERIA NCHINI.

TAASISI YA MSAADA WA KISHERIA AFRIKA (ALSF) KUWAJENGEA UWEZO WANASHERIA NCHINI.

Na Ramadhani Kissimba na Farida Ramadhani, Nairobi

SERIKALI ya Tanzania imeishukuru Taasisi ya Msaada wa Kisheria Afrika (ALSF) chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwajengea uwezo wataalam wa sheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hayo yameelezwa Juni mosi na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Amina Khamisi Shaabani kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba, baada ya kikao kati ya Tanzania na Taasisi ya Msaada wa Kisheria Afrika (ALSF) kilichofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.

 Amina amesema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali ya kisheria nchini katika usimamizi wa mikataba hususani ile inayohusika na utekelezaji wa miradi ya Ubia Kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).

“Tunaishukuru sana Taasisi hii kwa kuwajengea uwezo wataalam wa masuala ya Sheria husuani katika Taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,”amebainisha Amina.

Amesema pamoja na hayo, Taasisi hiyo pia inawajengea uwezo Maafisa katika Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Zanzibar, Dk. Juma Malik Akil, amesema wamejadiliana maeneo ambayo kwa Zanzibar bado yanahitaji msaada hususan katika kuwaongezea uwezo wa kusimamia mikataba wataalam walioko katika vikosi kazi mbalimbali vya majadiliano kati ya Serikali na wabia wa maendeleo.

Amesema kuwa vikosi kazi vinavyokuwa katika majadiliano na washirika wa maendeleo, Zanzibar vinahitaji kuongezewa uwezo katika maeneo yanayohusu mikataba ya uendeshaji wa miradi mikubwa ya serikali.

Naye, Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Frank Nyabundege, amesema Benki hiyo ni wanufaika wa huduma zinazotolewa na Taasisi ya Msaada wa Kisheria Afrika (ALSF) hususan masuala ya uwezeshaji wa kisheria.

“Sisi kama Benki tunahusika na mikopo, katika kutoa mikopo kuna mikataba na taratibu za ukusanyaji madeni ambavyo ni sehemu ambayo Taasisi hii imejikita kutujengea uwezo,”amesema Nyabundege.

Nyabundege, ameongeza kuwa, Taasisi hiyo ilitoa takribani Shilingi milioni 260 kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa sheria wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuhusu uandaaji wa mikataba na njia bora ya ukusanyaji wa madeni.

Taasisi ya Msaada wa Kisheria Afrika (ALSF) kwa muda mrefu imekuwa na program maalum nchini ya kuwajengea uwezo watumishi wa serikali na sekta binafsi hasa katika masuala mbalimbali ya kisheria,kwa upande wa majadiliano ya mikataba, ukusanyaji wa madeni ambayo yapo kwenye muktadha wa kisheria na changamoto zinazotokana na mikataba ya kibiashara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here