Angola
NAIBU Waziri wa Nishati Mheshimiwa Judith Kapinga amesema kuwa Tanzania imezindua Programu ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ya kuwasaidia Wanawake wa Afrika pamoja na Mkakati wake wa Kitaifa ikiwa na lengo la kuhifadhi mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kupunguza madhara ya kiafya, kupunguza mzigo wa mama na mtoto na ukatili wa kijinsia wakati wa kutafuta kuni na kuimarisha shughuli za kiuchumi na Kijamii ambapo ameelezea umuhimu wa Matumizi wa Nishati safi ya kupikia na matumizi mengine kwa Nchi za Afrika.
Kapinga ameeleza hayo Mei, 30 2024 Luanda Nchini Angola akimuwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko katika mkutano wa 42 wa Mawaziri wa Nishati na Maji wa Nchi za kusini mwa Afrika ( SADC) ambapo aliwaomba Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo kuunga mkono juhudi hizo zilizoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ameshauri Sekretarieti ya SADC kutambua juhudi zinazofanywa na nchi wanachama katika kuendeleza program na miradi mbalimbali ya mafuta na gesi inayotekelezwa na nchi hizo na kuratibu katika utafutaji wa rasilimali fedha kama inavyofanyika katika eneo la Nishati ya umeme.
Mkutano huo wa Mawaziri ambao ulitanguliwa na vikao vya Makatibu Wakuu pamoja na wataalam ulijadili hali ya uzalishaji na upatikanaji wa umeme katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika, uendelezaji wa nishati ya mafuta na gesi pamoja masuala ya maji.
Katika mkutano huo, Kapinga ameongozana na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga pamoja na Kamishna Msaidizi wa Mafuta na Gesi Mhandisi Joyce Kisamo kutoka Wizara ya Nishati.