Home KITAIFA SERIKALI YATOA SULUHU YA UVAMIZI MIGODINI, YAWAPATIA VIJANA MAENEO YA UCHIMBAJI WADOGO...

SERIKALI YATOA SULUHU YA UVAMIZI MIGODINI, YAWAPATIA VIJANA MAENEO YA UCHIMBAJI WADOGO NYAMONGO – MAVUNDE

Mara

SERIKALI imepanga kutenga maeneo ya uchimbaji na kuwapatia vijana ili wawe na sehemu ya kujipatia kipato ikiwa ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya uvamizi kwenye migodi mikubwa,

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipofanya ziara ya kikazi na kuzungumza na wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara katika eneo la Nyamongo, Wilayani Tarime.

Mavunde amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwa hataki kuona vijana wanahangaika kwa kujihusisha na uvamizi migodini kwa kukosa maeneo ya uchimbaji hivyo Wizara ya Madini tumeweka mkakati kupitia maeneo ambayo yamerudi Serikalini baada ya kufutwa leseni, wanaenda kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya kuwapatia vijana wachimbe madini na kuendesha maisha yao.

“Ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele katika fursa zilizopo kwenye madini. Serikali haifurahii hata kidogo uvamizi na migogoro mbalimbali inayojitokeza baina ya migodi na wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi hiyo,”amesema

Mavunde amebainisha kuwa tayari Wizara imefanya mazungumzo na Kampuni ya Barrick ili katika leseni zao za utafiti walizonazo katika maeneo ya Nyamongo, waweze kutenga eneo kwa ajili ya kuwapatia wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa awali wa kusaidia wachimbaji hao.

Vilevile, Waziri Mavunde ameahidi kwamba anakwenda kuielekeza STAMICO iweze kuleta mitambo Nyamongo katika maeneo ya wachimbaji wadogo yatakayotengwa kwa ajili ya kusaidia kuchoronga ili kuongeza tija kwenye uchimbaji wao.

Awali, ametolea ufafanuzi juu ya uvamizi migodini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwata Askari Polisi kuwa rafiki na jamii kwa ajili ya ulinzi wao na mali zao.

Akitoa salamu za wananchi wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara alipongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kutatua kero na changamoto za eneo la Nyamongo, na kuwaomba wananchi kuendelea kuiamini Serikali yao kwani itawaletea maendeleo ya kweli.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara,Kanali Evans Mtambi amewashukuru Mawaziri kwa kufika uwandani kutatua changamoto za wananchi na kuahidi kuendelea kusimamia maelekezo yote waliyotoa ili kuboresha maisha ya wananchi kwenye maeneo yanayozunguka migodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here